Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inapenda kuwajulisha wakazi wote wa Mkoa wa Tanga ambao wanaendela na zoezi la ujazaji wa fomu za Utambuzi na Usajili kwa awamu ya kwanza kuwa, Serikali imesikia kilio cha wananchi wake na hivyo inapenda kuwajulisha watendaji wote wa Serikali za mitaa ambao ndio wasajili kufungua vituo vya usajili saa 1.30 na kufunga saa 12.00 jioni.
Kwa kuwa zoezi hili lilitakiwa kukamilika tarehe 17/10/2014, Serikali imeongeza siku za usajili kwa lengo la kuweza kuwasajili wananchi wote ambao hawajasajiliwa. Aidha, wananchi wote wanaoweza kujaza fomu za Utambuzi na Usajili, waruhusiwe kuzijaza na msajili aweze kuzihakiki fomu hizo mbele ya mwombaji.
Kwa taarifa hii, Serikali inawahakikishia wananchi wote wa mkoa wa Tanga kuwa, wote watasajiliwa na hivyo inawaomba wote ambao hawajasajiliwa wajitokeze na kuwahi vituoni mapema kwa ajili ya kukamilisha zoezi la usajili wao. Napenda kuwahakikishia kuwa kila mtu mwenye stahili ya kusajiliwa atasajiliwa na kuwa kitambulisho cha Taifa ni haki ya msingi ya kila raia, mgeni mkaazi na mkimbizi mwenye umri wa miaka 18 na zaidi.
Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Imetolewa na:-
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)