Na Felix Mwagara, Nachingwea.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Mathias Chikawe ametangaza rasmi kuwa atagombea tena katika nafasi ya ubunge kupitia CCM katika uchaguzi Mkuu ujao na kulitetea jimbo lake. Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa CCM wa Wilaya na Kata ya Mtua, wilayani Nachingwea katika sherehe ya kuwapokea viongozi na wanachama wapya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliojiunga na CCM wilayani humo.
Waziri Chikawe alisema wananchi wake bado wanamuhitaji kwa hiyo hawezi kuacha kugombea nafasi hiyo kwani wazee na wananchi mbalimbali katika Kata zote alizokuwa akipita kufanya mazungumzo nao wanamuomba agombee tena nafasi hiyo.
"Wakati nikiingia ubunge mwaka 2005 katika jimbo hili kulikuwa hakuna lami na barabara nyingi za kwenda vijijini zilikuwa hazipitiki na pia maji yalikuwa shida lakini sasa barabara za lami mjini Nachingwea zimejengwa, maji yanapatikana tena yasio na chumvi, barabara vijijini zinapitika kwa kuwa zimechongwa vizuri kwa kuwawezesha wakulima kupitisha mazao yao," alisema Chikawe huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliofurika katika sherehe hiyo. Picha/Story na Felix Mwagara.