Sunday, October 26, 2014

BIASHARA HARAMU YA MKAA INAPOFADHILI UGAIDI




BIASHARA HARAMU YA MKAA INAPOFADHILI UGAIDI

Na Mwandishi Maalum, New York

Inaweza  ikawa ni  taarifa za  kushangaza kuwa hata mkaa ambao ni  nishati inayotumiwa na jamii kubwa sehemu mbalimbali hususani  Barani Afrika kwamba mapato yatokanayo na   biashara hiyo  yanaweza kuwa chanzo ya mapato kwa  makundi ya kigaidi.

Taarifa kwamba  mapato yatokanayo na mkaa yanatumika ndivyo sivyo, zimejidhirisha mwishoni  mwa wiki ( Ijumaa ) pale Baraza Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa lilipopitisha kwa kura  Azimio  namba  2182 la mwaka 2014 ambalo pamoja na mambo mengine linaweka vikwazo na  kupiga marufuku  biashara haramu ya mkaa  huko Somalia.

 Upigaji  marufuku hiyo na  vikwazo dhidi ya biashara ya mkaa  inatokana na kile kilichoelezwa   wakati wa   mkutano wa Baraza , kwamba kundi la kigaidi la Al- Shabaab limekuwa linanufaika na biashara hiyo kwa kuchukua sehemu ya mapato .

Azimio hilo  lilipita  kwa  kura  13  za  kuliunga mkono  huku  wajumbe wawili  Jordan na  Urusi  wakipiga kura ya kutoegemea upande wowote. Baraza linawajumbe  15 ambapo watano kati yao wanakura ya veto

Vikwazo dhidi ya  Biashara haramu ya  mkaa kutoka  Somalia iliwekwa kwa mara ya kwanza mwaka 2012 kwa azimio 2036.  Na    kwamba tangu kuwekwa kwa vikwazo hivyo  kumekuwapo na ongezeko la biashara  hiyo ya mkaa kiasi cha kuifanya Serikali ya Mpito nchin humo kulalamika kwa Baraza la  Kuu la Usalama.

Baadhi ya wajumbe waliozungumza baada ya kupitishwa kwa Azimio hilo ambalo pia linaongeza  muda wa vikwazo  vya   silaha, wameeleza kuwa  kundi la Al-Shabaab linapata theruthi moja ya mapato  yanayotokana na biashara hiyo ambayo inaeelezwa  kuwa thamani yake ni   dola za kimarekani 250 milioni.

Kupitia  Azimio hilo  Baraza linatoa wito kwa    wadau mbalimbali zikiwamo  nchi  zinazochangia walinzi wa Amani  nchini Somalia,  kupitia AMISOM kutoa ushirikiano katika  kudhibiti biashara hiyo  .

Aidha   Azimio linatilia mkazo wa ukaguzi wa meli zinazopita katika mwambao wa pwani ya Somalia na zile zinazopita katika  kina kirefu. Na  hasa pale inapohisiwa kwamba huenda zikawa zimebeba bidhaa hiyo  au silaha na zana nyingine za kivita ambazo zinadhibitiwa kupita Azimio hilo. Na kwamba bidhaa hizo   zikikamatwa basi viharibiwe mara moja.


Pamoja na  Azimio kutilia mkazo   vikwazo dhidi ya  biashara hiyo ya mkaa,  biashara ya haramu ya silaha  na au uingizaji wake. Pia  limeongeza muda wa  mamlaka kwa  Walinzi wa Amani wanaohudumu chini ya  Umoja wa Afrika ( AMISOM) hadi mwaka 2015.