| Bi. Shella Mbita, Mtoto                        wa Balozi Hashim Mbita nae pia alikuwa mmoja wa                        wajumbe waliohudhuria warsha ya amani na usalama                        jijini Arusha (Picha zote na Rosemary Malale)                        =============================================== 
 Na.                           Ally Kondo, Arusha 
 Warsha                          ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani                          Afrika iliyoandaliwa na Umoja wa Afrika (AU)                          imehitimishwa jijini Arusha siku ya Alhamisi                          tarehe 23 Oktoba 2014. Warsha hiyo ambayo                          kaulimbiu yake ilikuwa "Silaha zisitumike kuuwa                          watu Barani Afrika ifikapo mwaka 2020"                          ilimalizika kwa wajumbe kutoa Rasimu ya Tamko la                          Arusha (Arusha Declaration).   
 Katika                          Tamko hilo, kumebainishwa asili ya migogoro                          inayohusu nchi moja au baina ya nchi na nchi                          nyingine, vitu vinavyochochea migogoro na                          ukosefu wa utulivu Barani Afrika, wanaochochea                          na kudhamini migogoro pamoja na athari za                          maendeleo ya dunia kwa Bara la Afrika.  
 Aidha,                          Tamko hilo limeainisha juhudi zinazofanywa                          katika kukabiliana na vitendo vya siasa kali,                          uhalifu wa kimataifa na athari za mabadiliko ya                          tabianchi katika amani na usalama. 
 Tamko                          limebainisha pia kuwa migogoro mingi katika nchi                          za Afrika inasababishwa na ukosefu wa utawala                          bora katika Serikali, uwajibikaji, uwazi,                          uongozi shirikishi pamoja na kushindwa kutatua                          changamoto za umasikini na ukosefu wa usawa. 
 Kwa                          mujibu wa Tamko hilo, wajumbe kwa kauli moja                          walikubaliana na hoja kuwa ili nchi za Afrika                          ziondokane na matatizo hayo, hazina budi                          kutekeleza miongozo na maamuzi yanayotolewa na                          AU kuhusu amani, usalama na uongozi. Walisema                          kuwa maamuzi hayo yanatoa dira nzuri ya namna ya                          kukabiliana na changamoto za usalama Barani                          Afrika, isipokuwa nchi za Afrika hazina                          utamaduni wa kuyatekeleza. 
 Hivyo,                          wajumbe walisisitiza umuhimu kwa nchi wanachama                          wa AU kutekeleza maamuzi yote yanayofanywa na                          kuridhiwa na AU, Jumuiya za Kikanda na wadau                          wengine.  
 Aidha,                          walitoa wito kwa nchi wanachama wa AU, Kamisheni                          ya AU, Jumuiya za Kikanda, Baraza la Amani na                          Usalama la AU na wadau wengine kulipa kipaumbele                          suala la kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya                          utekelezaji wa maamuzi hayo. 
 Sanjari                          na hayo, wajumbe walipongeza mabadiliko chanya                          yanayotokea Barani Afrika ikiwa ni pamoja na                          kupungua kwa migogoro ya kutumia silaha,                          kuongezeka kwa chaguzi za kidemokrasia, kukua                          kwa uchumi na ongezeko la kasi ya kupambana na                          vitendo vya ufisadi katika nchi nyingi za                          Afrika. 
 Licha                          ya maboresho hayo, wajumbe walielezea wasiwasi                          wao   kuhusu tishio linalotokana na changamoto                          mpya katika amani na usalama wa Bara la Afrika.                          Walihimiza umuhimu wa kutumia mbinu za kibunifu                          kukabiliana na changamoto hizo ambazo ni;                          uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uharamia,                          biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha                          na dawa za kulevya na biashara ya fedha haramu. 
 Wakati                          wa kufunga warsha hiyo ambayo iliwakutanisha                          Mabalozi, wasuluhishi, wajumbe maalum,                          wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na wasomi                          mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe.                          Mnasa Nyerembe alielezea matumani yake kuwa,                          washiriki walipata fursa nzuri ya kujadili kwa                          kina chanzo cha migogoro Barani Afrika na                          kupendekeza njia muafaka za kukabiliana nayo.                          Alisisitiza umuhimu wa mapendekezo hayo                          kuingizwa katika sera za kitaifa, kikanda na                          kimataifa ili yaweze kuwa na manufaa.  
 -Mwisho- |