Sunday, October 12, 2014

Usajili Vitambulisho vya Taifa wabishahodi Ruvuma


Usajili Vitambulisho vya Taifa wabishahodi Ruvuma
 Na Thomas William 
 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekutana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuweka mpango kazi madhubuti wa usajili wa watu katika mkoa huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27, 2014. 
 Akifungua kikao hicho cha kazi Oktoba 11, 2014, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Joseph Mkirikiti amesema viongozi wa wote wa mkoa huo wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo lenye manufaa makubwa kiuchumi, kijamii na ulinzi na usalama wa Taifa letu. 
 Amesema viongozi wote wa wilaya, tarafa, kata na kijiji wanatakiwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye usajili na kusimamia mwenendo mzima wa usajili katika maeneo yao ya utawala. 
 Mkirikiti amewataka viongozi wote kuwa wazalendo kwa kuhakikisha kwamba wasio Watanzania hawapati vitambulisho wanavyopewa Watanzania ikizingatiwa kwamba mkoa huo umepakana na nchi za Malawi na Msumbiji. 
 Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Paya Hamphrey amesisitiza viongozi hao kutekeleza jukumu la usajili kwa kuwa lipo kisheria na ni wajibu wa kila kiongozi wa wilaya, tarafa, kata na kijiji kusimamia sheria za nchi. 
 Akitoa taarifa ya utekelezaji ya NIDA, Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho, Paul Bwathondi amesema mamlaka inaendelea na usajili wa watu hivi sasa imekwishasajili Zanzibar, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, inaendelea na usajili Tanga na baadaye Ruvuma na Kilimanjaro. Aliwaomba viongozi hao kutoa elimu kwa wananchi wao hasa kuandaa viambatisho muhimu vinavyothibitisha uraia, umri na makazi kama vile, vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya elimu, pasi ya kusafiria, namba ya utambulisho ya mlipakodi, kitambulisho cha mpigakura na cheti cha bima ya afya na kitambulisho cha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
 Pia amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hili na wananchi katika mikoa mingine ambao haijafikiwa kuvuta subira kwani wote watafikiwa kulingana na ratiba ya mamlaka.
Juu na chini ni  Washiriki wa kikao kazi cha kuweka mkakati wa utambuzi na usajili wa watu wakiendelea na kikao, katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Songea, Ruvuma Oktoba 11,2014.