Picha ya pamoja ya washiriki wa Warsha ya kujenga uwezo kwa maafisa wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali. Kutoka kushoto (waliokaa) ni Bw. Styden Rwebangila kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Bi.Anna Shakarova ambaye ni Mkurugenzi wa Program wa Maendeleo ya Kiuchumi, Bw. Yohane Masara –Kaimu Mkurugenzi,Divisheni ya Mikataba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(katikati),Bw.Steven Sparling na Bi Clare Power kutoka Kampuni ya Uwakili ya K&L Gates ambao ni wawezeshaji wa Mafunzo hayo.
Bi.Anna Shakarova ambaye ni Mkurugenzi wa program ya Maendeleo ya Kiuchumi ya ISLP akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada wakati wa mafunzo hayo.Kutoka kushoto ni Bw.Mikidadi Rashidi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Bw.Juma Karibona(kati) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu -Zanzibar na kulia ni Bw.Patric Malogoi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeendelea kuwajengea uwezo watumishi na wataalam katika maeneo ya sekta ya madini na gesi asilia kwa lengo la kuimarisha uwezo wa wataalam hao katika kuandaa, kujadili na kusimamia miradi mikubwa na mikataba ya gesi asilia nchini.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Yohane Masara wakati akifungua mafunzo yaliyojumuisha Maafisa kutoka Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali yanayofanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba,2014.
Bw.Masara ameeleza kuwa eneo la gesi asilia ni jipya kwa nchi yetu na hivyo mafunzo haya yatasaidia katika kujenga uwezo wa wataalam juu ya namna ya kufanya majadiliano na kuingia mikataba itakayoleta tija na kuchangia katika Maendeleo ya Tanzania.
Akisisitiza Umuhimu wa mafunzo hayo, Bw. Masara alieleza kuwa pamoja na mchango ambao umekuwa ukitolewa na Sekta hii katika Maendeleo na uchumi wa nchi, kumekuwepo na malalamiko na hoja mbalimbali za msingi kuwa mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini ambayo Serikali za nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa zikiingia, ikiwemo Tanzaina haina ulingani sawa(win-win situation) hivyo kupelekea nchi husika kupata maslahi duni kutokana na uwekezji huo ambapo pia alieleza kuwa hali hii imekuwa ikipelekea baadhi ya nchi kuingia katika migogoro ya kiuchumi na mara nyingine vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kugombania rasilimali.
Serikali ya Tanzania kwa kulitambua suala hilo na katika kutatua Changamoto za aina hii, imekuwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao wamekuwa wakitupatia msaada wa fedha pamoja na wataalam wa masuala mbalimbali kuandaa mafunzo maalum kwa Maofisa na wataalam wa Serikali wa ngazi mbalimbali kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inapata utaalam stahiki hususani katika maeneo mapya ya mafuta na gesi.
Aidha Bw. Masara aliwataka washiriki kutambua kuwa Tanzania inayo maeneo ya kipaumbele ambayo ingependa kufaidika nayo kutokana na uwepo wa rasilimali zilizopo hivyo kuwa makini wakati wa kufanya majadiliano ya mikataba mbalimbali ambapo aliongeza kuwa mikataba ikijadiliwa vizuri itachangia katika kuongeza thamani ya rasiliamali tulizonazo kwa njia ya mitaji,teknolojia na ujuzi,mapato yanayotokana na kodi,fedha za kigeni zinazotokana na biashara ya rasilimali hizo,kupanua wigo wa ajira na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Bi. Anna Shakarova, ambaye ni Mkurugenzi wa Program wa Maendeleo ya Kiuchumi ya Program ya Kimataifa ya Wanasheria Waandamizi (International Senior Lawyers Project) alieleza kuwa, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limekuwa likifanya kazi na nchi za Kiafrika kupitia Program hiyo katika masuala ya kujenga uwezo na kuhakikisha kuwa nchi husika zinafaidika na rasilimali zake kwa kutoa mafunzo kwa maafisa wa ngazi mbalimbali katika maeneo ya mikataba,masuala ya kodi,uchimbaji wa madini,mafuta na gesi. Bi. Shakarova aliongeza kuwa Program hii imekuwa ikitafuta walimu na wataalam kutoka katika kampuni kubwa za Kisheria za Kimataifa ambao hujiunga na Program hiyo na huwawezesha wataalam hao kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani zikiwemo nchi za Kiafrika kama Tanzania na nyinginezo.
Akitoa ufafanuzi wa maeneo ambayo yatahusika katika mafunzo hayo, Bw. Steven Sparling ambaye ni mmoja wa waezeshaji kutoka kampuni ya Uwakili ya K&L ya nchini Marekani,alieleza kuwa maandalizi ya miradi mbalimbali katika eneo la mafuta na gesi yanahitaji umakini mkubwa na uelewa ili kuhakikisha kuwa kila upande unaohusika unaridhirika na makubaliano ambayo yatafanywa na hatimaye kuingia mikataba yenye tija kwa nchi husika.
Aidha Bw.Sparling aliwathibitishia washiriki wa mafunzo hayo kuwa atatumia uzoefu wake wa zaidi ya miaka kumi na tano (15) alionao katika eneo hili la gesi asilia (liquefied natural gas) kuhakikisha kuwa wanapata mbinu madhubuti za namna ya kujadili na kusimaia miradi na mikataba katika eneo hilo.
Naye Bi.Clare Power,ambaye ni miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo hayo alisisitiza kuwa ni vyema washiriki wa mafunzo wakaonesha ushirikiano wakati wa kujifunza kwa kuuliza maswali na kuibua mijadala ambayo itachangia katika kuimarisha uelewa. Bi. Power ,vilevile aliahidi kutoa ushirikiano na uzoefu wake alionao katika kufanya kazi na Serikali za nchi mbalimbali duniani katika kuhakikisha kuwa kila mshiriki wa mafunzo hayo anapata uelewa katika usimamizi wa masuala ya gesi asilia ili kuhakikisha kuwa mikataba itakayohusika katika maeneo hayo inakuwa na maslahi kwa nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Akihitimisha hotuba ya ufunguzi,Bw. Masara alisema kuwa mafunzo hayo ya yanajumuisha maafisa na wataalam kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania Bara na Zanzibar,Wizara ya Nishati na Madini (MEM),Wizara ya Fedha (MOF),Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandaji wa mafunzo hayo ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Nishati na Madini,pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Program ya Kimataifa ya Wanasheria Waandamizi (ISLP) ambao wamekuwa wakiipatia Serikali ya Tanzania msaada na ushirikiano katika eneo la kujenga uwezo na kuwapatia elimu Maafisa na wataalam mbalimbali wa Serikali ya Tanzania.