Friday, October 31, 2014

Rais Kikwete amtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa arusha kufuatia vifo vya watu katika ajali iliyotokea jijini humo





Rais Kikwete amtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa arusha kufuatia vifo vya watu katika ajali iliyotokea jijini humo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Magesa Mulongo kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 30 Oktoba, 2014 katika eneo la Makumira Wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha na kusababisha vifo vya abiria 12 papo hapo na wengine kujeruhiwa. 

 "Nimeshtushwa na kusikitishwa sana kutokana na ajali hii mbaya ambayo kwa ghafla imeondoa uhai wa wenzetu 12 wasio na hatia kutokana na kukosekana kwa umakini wa binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto katika barabara zetu", amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Ameongeza Rais Kikwete: "Kutokana na ajali hiyo, naomba upokee Salamu zangu za Rambirambi, na kupitia kwako, Salamu hizi na pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao.  Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina".

Aidha, Rais Kikwete amewapa pole sana wote walioumia katika ajali hiyo akimwomba Mwenyezi Mungu awape ahueni ili wapone haraka na kuweza kurejea katika shughuli za maendeleo yao na yale ya taifa. "Naomba Mwenyezi Mungu awajalie ahueni ya haraka, ili muweze kupona haraka na kurejea katika maisha yenu ya kujitafutia riziki na kuchangia maendeleo ya taifa letu."

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
31 Oktoba,2014