Bw. Clement Ngosha wa kijijini Kabita Wilayani Busega, Simiyu, akitumia mbegu za mahindi kueleza hali ya chakula kijijini hapo kwa wataalam wa Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Oktoba, 2014.
Mtaalam wa Usalama wa chakula kutoka Wizara ya kilimo, chakula na Ushirika, Bi. Tatu Kayumbu akiihoji moja ya kaya kijijini Mwamanyili,Wilayani Busega, Simiyu wakati wa Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kijijini hapo, Oktoba, 2014.
Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Kabita wilayani Busega, Simiyu wakifuatilia mkutano wa kijiji uliokuwa ukijadili hali ya Chakula na Lishe kijijini hapo wakati Ofisi ya Waziri Mkuu ilipofika kijijini hapo kufanya tathmini ya masuala hayo Oktoba, 2014.
Na. Ibrahim Hamidu
Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa maafa inafanya Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe Mkoani Simiyu katika Wilaya zake zote ambazo ni; Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa ,Bariadi Meatu na Busega.
Akiongea mkoani Simiyu kiongozi wa Wataalam wa tathmini ambaye pia ni mratibu wa shughuli za maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Edgar Senga alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imefikia maamuzi hayo ya kufanya tathmini mkoani Simiyu baada ya mkoa huo kutuma maombi katika Ofisi hiyo kuwa wana upungufu wa chakula.
" Ofisi ya mkoa ya Simiyu ilileta maombi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wanaoupungufu wa chakula takribani tani 48,975, kwa kuwa Ofisi yetu ndio yenye dhamana ya kuratibu misaada ya chakula hivyo haikuwanabudi kufanya tathmini ya haraka ili kubaini hali ya chakula ya mkoa huu ili kuweza kuamua namna ya kushughulikia maombi yao ya msaada wa chakula" alisema Senga
Senga alibainisha kuwa Wataalam wa tathimini hiyo wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika Idara ya Usalama wa Chakula ambao kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wametawanyika katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ambapo katika kila Wilaya vitachaguliwa vijiji vitatu vya kufanyiwa tathmini.
"Katika kila kijiji wataalamu hawa watakuwa wanamadodoso ya Wilaya na kijiji ambayo yatasaidia kutoa taarifa mahsusi za hali ya chakula na Lishe katika ngazi ya Wilaya na Kijiji, lakini pia wataalamu wanayo madodoso ya kaya ambayo yanalenga kupata taarifa za hali ya chakula na Lishe kwa kaya husika kwa vijiji vitakavyoteuliwa na Serikali za vijiji hivyo.
Kwa kuzingatia kuwa wataalam wa masual ya chakula katika ngazi ya Wilaya watakuwa wanahusishwa ninaamini tutapata taarifa bora ya hali ya chakula ya mkoa wa Simiyu " alisisitiza Senga.
Akiongea Ofisini kwake alipotembelewa na ujumbe wa Wataalamu hao Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) mkoani Simiyu, Bw. Joseph Nandira alibainisha kuwa Katika kipindi cha msimu wa 2013/2014, Mkoa ulijiwekea malengo ya kuzalisha jumla ya tani 1,003,578 za mazao ya chakula aina ya nafaka/wanga na tani 150,257 aina ya mikunde. Mavuno halisi yaliyopatikana ni tani 476,024 za chakula aina ya nafaka/wanga na tani 74,944 za chakula aina ya mikunde.
Nandira alibainisha kuwa kutokana na tabia ya wananchi kuuza sehemu kubwa ya chakula ili kukidhi mahitaji ya familia zao, tathmini ya hali ya chakula tuliyoifanya mwezi Julai 2014, tulibaini kuwa Mkoa Unaupungufu wa chakula wa tani 48,975 za nafaka ambao umeanza kuanzia mwezi Oktoba na upungufu huo wa chakula unatarjiwa kuwepo mwezi Novemba/Desemba hadi Februari, 2015 kama wilaya hazitapata msaada wa chakula.
"Tathmini hiyo ilibaini Halmashauri za Wilaya za Busega na Meatu zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Agosti, 2014 hadi Februari, 2015. Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa na Bariadi Mji zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Oktoba, 2014 hadi mwezi Februari, 2015. Ili kukidhi haja ya upungufu wa chakula ndio maana tuliomba jumla ya tani 48,975 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu." Alisema Nandira
Nandira alifafanua kuwa ili kuhakikisha tatizo la upungufu wa chakula linakwisha tayari mkoa unayomikakati ambayo inajikita katika Kuwahimiza wananchi kutumia vizuri chakula kilichopatikana na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu makadirio ya mahitaji ya chakula ngazi ya kaya kwa mwakapamoja na Kuwashauri wananchi kuuza sehemu ya mifugo yao na kujinunulia chakula wakati huu ambapo chakula bado kina bei ndogo na kinapatikana ndani ya Wilaya na Mkoa.
Aliongeza kuwa mkoa unaendelea kuwashauri wananchi kujinunulia chakula kutokana na fedha za mauzo ya pamba. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi bora ya chakula, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili chakula kisibunguliwe na wadudu. Kuwashauri wananchi kuuza ziada ya chakula walichovuna na si vinginevyo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2012 mkoa wa Simiyu una jumla ya watu 1,584,157 ambao wanahitaji jumla ya tani 404,752 za chakula aina ya nafaka/wanga na tani 144,553 za chakula aina ya mikunde kwa kipindi cha msimu wa mwaka 2013/2014.