Mbunge wa Jimbo la Kawe, Mhe Halima Mdee |
Habari na Mwene Said
wa Globu ya Jamii
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeagiza Mbunge wa Jimbo la Kawe, Mhe Halima Mdee (35) na wenzake wawili kufika mahakamani ili iweze kuanza kusikiliza kesi inayowakabili ya kupinga amri halali ya Jeshi la Polisi na kukusanyika isivyo halali kwa lengo la kwenda Ikulu.
Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa mshtakiwa wa kwanza Mdee, wa tatu, Renina Leafyagila na wa sita Sophia Fanuel kutoa kushindwa kufika mahakamani.
Wakili wa Serikali Mohamed Salum alidia kuwa upande wa Jamhuri uko tayari kuendelea kusikiliza maelezo ya awali na kwamba hauna taarifa za washtakiwa hao. Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa wadhamini wa washtakiwa wana taarifa za washtakiwa.
Mdhamini wa Mdee alidai kuwa alikuwa kwenye ziara za kichama kanda ya ziwa na kwamba alipanga kurejea jijini jana lakini ilishindikana baada ya ndege kuahirisha safari jana (juzi). Mdhamini wa mshtakiwa wa tatu, alidai kuwa mshtakiwa huyo amefiwa na baba yake mzazi na kwamba leo (jana) walikuwa wanafanya maziko.
Halikadhalika mdhamini wa mshtakiwa wa sita, alidai kuwa mshtakiwa yuko kwenye msafara wa ziara ya chama na Mdee na kwamba walikosa usafiri wa ndege kurejea jijini Dar es Salaam.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa sababu ya mshtakiwa wa tatu ni ya msingi kwa sababu kufa hakuna taarifa.
"Mheshimiwa hakimu sababu ya mshtakiwa wa kwanza na wa sita hazina msingi na kwamba mahakama isipokemea itakuwa changamoto ya kuruhusu kila mtu kufanya anavyotaka na kuchelewesha usikilizwaji wa kesi… suala la kufika mahakamani washtakiwa kusikiliza kesi yao ni la msingi na kwamba ziara za kichama hazina uhusiano na mahakama hii "alidai Salum.
Mhe. Hakimu Kaluyenda alisema wadhamini wahakikishe washtakiwa wanazingatia umuhimu wa kuhudhuria mahakamani na kwamba siku mbili kabla ya kesi wanatakiwa kufanya mawasiliano nao ili kuzuia ucheleweshaji wa kusikilizwa kesi yao.
Alisema washtakiwa wanatakiwa kuwepo mahakamani kila kesi yao inapopangwa na alipanga kusikiliza maelezo ya awali Novemba 5, mwaka huu. Mbali na Mdee, Leafyagila,Fanuel,wengine walioachiwa huru ni Rose Moshi, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatus Mmari. Oktoba 7, mwaka huu, Mdee na washtakiwa wenzake, walishindwa kutimiza masharti ya dhamana, baada ya nyaraka za wadhamini kushindwa kukamilika kufanyiwa uhakiki na hivyo kulazimika kulala mahabusu siku moja.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika Mtaa wa Ufipa, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam, isivyo halali, washtakiwa walikiuka amri halali ya Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel Tillf, iliyowataka kutawanyika.
Ilidaiwa kuwa siku na mahali pa tukio la kwanza, washtakiwa walifanya mkusanyiko isivyo halali kwa lengo la kuandamana kwenda Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Washtakiwa wote walikana mashitaka hayo.