Na Beatrice Lyimo- MAELEZO,Dar es salaam.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatarajia kufanya kampeni shirikishi ya ugonjwa wa Surua na Rubella kuanzia tarehe 18 hadi 24 oktoba, 2014.
Akizungumzia kampeni hiyo itakayofanyika nchini nzima leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Donan Mmbando amesema kuwa itawahusisha watoto wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka 15.
Amesema kampeni hiyo itaambatana na utoaji wa matone ya Vitamini A, dawa za kutibu na kukinga magonjwa ya Minyoo, Usubi,Matende na Mabusha.
Dkt. Mmbando amesema kuwa lengo na madhumuni ya kampeni hiyo ni kudhibiti milipuko ya magonjwa ya Surua na Rubella ili kupunguza vifo na madhara yanayosababishwa na magonjwa hayo.
"Katika kampeni hii tutatoa dawa za kutibu na kukinga magonjwa ya Minyoo, Usubi, Matende na Mabusha katika mikoa 16 yenye maambukizi makubwa ya magonjwa haya", Amesisitiza Dkt. Mmbando.
Amefafanua kuwa chanjo ya Surua na Rubella itatoa fursa ya kutoa kinga kwa watoto wengi zaidi ambao hawakupata chanjo hiyo utotoni katika mikoa yenye maambukizi makubwa ya magonjwa hayo ambayo ni Mtwara, Lindi, Tanga , Dar es salaam,Morogoro, Pwani, Tabora, Manyara, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Singida, Dodoma na Njombe.
Akitoa ufafanuzi kuhusu chanjo hizo amesema kuwa chanjo ya Surua na Rubella itatolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 9 hadi chini ya miaka 15, matone ya vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi chini ya miaka 5.
Nyingine ni dawa za minyoo (Mebendazole) zitakazotolewa kwa watoto wenye umri wa miezi 12 hadi chini ya miaka 5 nchi nzima na dawa za kutibu na kukinga minyoo (Albendazole) Usubi, Matende na mabusha au Ngirimaji kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 5 na kuendelea katika mikoa 16 iliyobainishwa.
Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Dafrosa Lyimo ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao katika vituo vya afya ili waweze kupata chanjo hiyo.
Pia ametoa wito kwa mama wajawazito kuhakikisha kuwa wanapata chanjo ya Surua-Rubella ili kuwakinga watoto wao dhidi ya matatizo ya Moyo, mimba kuharibika, kujifungua kabla ya wakati na mtindio wa ubongo yanayotokana na ugonjwa huo.