Saturday, October 11, 2014

ADHA YA UKEKETAJI TANZANIA KUJADILIWA NA WABUNGE UINGEREZA


ADHA YA UKEKETAJI TANZANIA KUJADILIWA NA WABUNGE UINGEREZA
Na Freddy Macha

Jumatano ijayo tarehe 15 Oktoba, 2014...kundi la kina mama watatu akiwemo Mtanzania litashiriki jopo la ukeketaji na Wabunge, London, Uingereza.

Mtanzania, Rhobi Samwelly, mama wa watoto wanne, ni mzawa wa Butiama, Mara. Wenzake ni Comfort Momoh, toka Nigeria, anayetibu wanawake waliokeketwa hospitali mbili za Guy's na St Thomas, London na Ann-Marie Wilson mkurugenzi wa "28 Too Many." Shirika hili lenye tovuti yenye http://28toomany.org/ ni maktaba kubwa yenye habari, picha, utafiti na uchunguzi wa ukeketaji duniani.
Bango linalotumika kuchangia makutano na hafla mbalimbali za fedha za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana Mugumu, Mara

Mwaka1997 Comfort Momoh alianzisha msururu wa shughuli za kuwasaidia akina mama waliokeketwa likiwemo shirika la African Well Women's Clinic. Bi Momoh mwenye shahada ya uzamili (MA) ni mshauri wa shirika la Afya duniani (WHO) kuhusu adha ya ukeketaji.

Mtanzania Rhobi na Ann-Marie walikuwa baadhi ya wazungumzaji kwenye hafla iliyofanywa Alhamisi na Jumamosi iliyopita kuchanga fedha za kujenga nyumba ya hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji, Mugumu, Mara.

Hafla hiyo iliendeshwa na shirika la urafiki baina ya Tanzania na Uingereza (British Tanzania Society) na Shirika la Misaada ya Kimaendeleo Tanzania (Tanzania Development Trust Fund). Fedha zilizokusanywa zinaendelea kusaidia ujenzi wa nyumba ya kuwahifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji jimbo la Mara.
Mwanasaikolojia, mtafiti na mtetezi wa haki za waliokeketwa, Anne-Marie Wilson(kulia kabisa) akijadiliana na wanachama wengine wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs), ukumbi wa Central Hall, Westminster baada ya hotuba yake. Alisisitiza kila sekunde kumi , msichana fulani hukeketwa ulimwenguni. Kati kati ni mweka hazina wa BTs, Bw. Robert Gibson na Jonathan Cape, mwendeshaji wa hafla.

Nilimuuliza Dada Rhobi je hawa wasichana hawatadhurika? Je, wazazi husika hawatawafuata? Akajibu kwa sasa kuna vyombo vingi husika kikiwepo polisi, serikali na kanisa la Anglican ambalo yeye ni mjumbe pia.

Rhobi ni mratibu wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya akina mama vijiji vya Mara. Mbali na ukeketaji anaangalia pia maslahi ya unyanyasaji wa kijinsia. Baada ya Bi Neema Wambura kupigwa na mumewe majuma kadhaa yaliyopita, Bi Rhobi alikuwa mmoja wa waliomhudumia kwa kuhakikisha anapata matibabu. Neema alimwagiwa maji moto na kuunguzwa kifuani na mkononi.

Kufuatana na maelezo ya dada Rhobi na Ann-Marie leo hii wastani wa wasichana wanaokeketwa ni miaka minane hadi kumi na nne. Ila wapo wazazi wanaowapeleka watoto wenye miaka miwili.

Nchi 29 duniani ikiwemo Tanzania bado zinakeketa wasichana. Licha ya kufanywa vilema, kujifungua kwa shida, kupata maumivu ya daima wakati wa haja ndogo na hedhi, baadhi ya wasichana hufa.

Dada Rhobi Samwelly: "Msichana anapokufa mwili hutupwa tu vichakani na kuliwa na wanyama. Huwa siri. Wanaficha. Mama aliyefiwa huwambiwa asilie, asiwaambie watu. Ni aibu. Asiomboleze. Asilie. Ni mkosi. Balaa."

Kawaida kipindi cha ukeketaji ni miezi ya Novemba na Desemba, kila miaka miwili. Wasichana wanaokimbia adha hii wamekuwa wakilindwa na kanisa na sehemu nyingine. Yumkini nyumba inayojengwa Mugumu itakuwa mkombozi wao. Gharama zake zimekadiriwa kuwa takribani paundi 60, 000 za Uingereza. Paundi moja na shilingi elfu mbili na kitu.

Ukeketaji ambao unajulikana dunia nzima kwa jina FGM (female genital mutilation) huwa wa aina nne. Aina iliyoenea ni kuondoa kinembe, kuondoa midomo ya uke, tatu kuondoa kinembe na midomo. Aina hizi tatu za kukeketa zina lengo za kupungusa kabisa hisia za ngono na mapenzi ya mwanamke. Desturi iliwekwa ili wanawake wasitembee ovyo nje ya ndoa, wawe tu wazazi na mali za waume zao. Ya nne ni kuondoa kila kitu na kubakisha tundu la haja ndogo na mfereji wa damu siku za hedhi.

Mwanamke anapojifungua hupasuliwa akishamaliza hushonwa tena. Utaratibu huo huendelea maisha yake yote ya uzazi. Wanawake husika hutembea na maumivu usiku na mchana maisha yao yote. Ngono, mapenzi, uzazi vyote si furaha kwao. Si kweli ukeketaji ni suala la dini. Ulikuwepo kabla ya dini tunazofuata toka Mashariki ya Kati zilipoingia.

Moja ya kazi za muuguzi Comfort Momoh ni kusaidia wanawake hawa. Licha ya nchi 29 za Kiafrika, Mashariki ya Kati na bara Asia, nchi za Kizungu za Ulaya, Marekani, Canada na Australia pia zinao wahamiaji wanaoendesha shughuli hizi. Kisheria ukeketaji unakatazwa lakini utekelezaji haujawa makini.

Mwezi Juni, Kamishna wa Haki za Binadamu, Umoja wa Mataifa Navi Pillay alisisitiza ukeketaji hauna faida zozote za kiafya. Ukeketaji alifafanua Bi Pillay, "unaathiri maisha na kuhatarisha maisha ya watoto waliozaliwa na kina mama walioupitia."

Bi Pillay alisisitiza kwamba vita au mapambano dhidi ya ukeketaji ni kazi yetu sote wanaume, wanawake, watoto, vijana kwa wazee.Bila kuchagua umri, jinsia au rangi.

Jopo la Jumatano, Bungeni Uingereza, litakuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo la Stafford, Jeremy Lefroy, ambaye anawakilisha chama cha Conservatives. Bwana Lefroy pia huendesha shirika la ufadhili wa maendeleo Equity Africa lenye dhamira ya kupunguza umaskini barani.

Wazungumzaji wengine ni Lynne Featherstone, Mbunge anayewakilisha serikali kwa ajili ya shirika la Kimaendeleo ya Kimataifa Uingereza (DFID).Mwaka jana DFID ilijitolea kiasi cha paundi 35 milioni kupunguza ukeketaji duniani kwa asilimia 30.
-London, 10 Oktoba 2014.
Anna Marcus, wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs) akishangilia bendera za Tanzania.
Janet Chapman & Jonathan Cape Waingereza wanaojali maendeleo ya Watanzania. Wameendesha maonyesho matatu mwaka huu mjini London, kusaidia mchango wa fedha za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana wanaokimbia ukeketaji , Mugumu, Mara.
Mheshimiwa Jeremy Lefroy, Mbunge wa jimbo la Stafford, Uingereza. Atasimamia jopo la Jumatano ijayo. Picha toka tovuti yake.
Bi Rhobi Samwelly (katikati) akiwa na mkewe Balozi wetu Uingereza, Mama Joyce Kallaghe(kushoto) na Bi. Mariam Kilumanga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania, Uingereza (TAMWA). Hafla ya kukusanya fedha kusaidia ujenzi wa kituo cha wasichana wanaokimbia ukeketaji Mugumu, Mara.
Rhobi akiwa na Fahma (kushoto) mzungumzaji mwingine toka Afrika aliyekemea Ukeketaji.
Wasikilizaji wa kilichokuwa kikiongelewa. Pichani ni Tony Janes aliyefanya kazi Tanzania miaka ya zamani. Siku hizi kastaafu.