Monday, September 22, 2014

WAZIRI MBARAWA ATILIANA SAINI MKATABA WA UTENDAJI NA WENYEVITI WA BODI ZA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA MAWASILIANO



WAZIRI MBARAWA ATILIANA SAINI MKATABA WA UTENDAJI NA WENYEVITI WA BODI ZA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA MAWASILIANO
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Prof. Makame Mbarawa ameongoza zoezi la utiaji Saini Mkataba wa Utendaji baina yake na Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zao kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Lengo la Mhe. Waziri kuwekeana saini Mkataba wa Utendaji na Wenyeviti wa Bodi ni kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Wenyeviti wa Bodi hizo ili kuleta ufanisi na tija kwenye Sekta ya TEHAMA, Sayansi na Teknolojia ili iweze kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na mchango wa sekta kwenye pato la Taifa.

Aidha, Mhe. Mbarawa alisema kuwa mapitio ya utekelezaji wa mkataba huo utafanyika kila baada ya miezi mitatu ili kufuatilia namna unavyotekelezwa na kubaini changamoto zinazowakabili wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Taasisi zilizo chini ya Wizara ni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Kampuni ya Simu Tanzania, Shirika la Posta Tanzania, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Tume ya Nguvu za Atomii Tanzania na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Prof. Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa Utiaji Saini Mkataba wa Utendaji baina yake na Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zao kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote,Prof. John Nkoma akiweka saini mkataba wa utendaji baina yake na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Mhe. Prof. Makame Mbarawa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Mhe. Prof. Makame Mbarawa akipeana mkono na Prof. Nkoma baada ya kuwekeana saini mkataba.