Mmoja kati ya waandaaji wa Serengeti Fiesta 2014, Musa Hussein akizungumza na na waandishi wa habari kuhusu Fiesta itakayofanyika Mkoa wa Mbeya uwanja wa Sokoine Jumapili. LILE bonanza lililokuwa likisubiriwa kwa hamu na wakazi wa Mbeya, Serengeti Fiesta, sasa linatarajiwa kuanza kutingisha viunga vya jiji la Mbeya kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 28, Septemba mwaka huu. Akizungumza na vyombo vya habari, mmoja wa waandaaji wa Serengeti fiesta 2014,Musa Hussein,alisema mwaka huu wameboresha kwa kuongeza vipengere kadhaa vitakavyofanyika kabla ya siku yenyewe. Hussein alisema Septemba 26, siku ya Ijumaa kuanzia majira ya saa nane mchana kutakuwa na Fiesta Soccer Bonanza litakalofanyika katika viwanja vya Chuo cha uhasibu(TIA) Mafiati jijini Mbeya. Alisema katika bonanza hilo litashirikisha timu nne za mabaa na timu moja ya Chuo cha Uhasibu ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia Katoni 10 za Bia aina ya Serengeti huku mshindi wa Pili akiambulia Katoni Tano. Alizitaja timu hizo kuwa ni Chuo cha Uhasibu(TIA), Baa ya Kalembo, Baa ya Tugelepo na Mabatini Salalizya baa ambapo bonanza hilo litaendeshwa kwa mtindo wa mtoano. Hussein alisema siku itakayofuata kutakuwa na sherehe kabla ya Fiesta(Pre Party) itakayofanyika katika ukumbi wa Bab'z Lounge ambapo wasanii wote wakaokuwepo siku ya Serengeti watahudhuria pamoja na timu nzima ya Clouds media. Alisema siku hiyo kutakuwa na kiingilio cha Shilingi 10,000 kwa kila mtu huku watu 50 wa kwanza watapata tiketi bure ya kuingilia Jumapili kwenye Fiesta yenyewe. Aliongeza kuwa Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili kutakuwa na shindano la kupata waimbaji wa kike(Serengeti super nyota Diva) ambapo mwenye kipaji anatakiwa kuchukua fomu bure Generation fm. Alisema mshindi wa kwanza katika shindano hilo atasafirishwa hadi Dsm kwenye fainali pamoja na washindi wa mikoa mingine 18 kumpata mshindi mmoja atakayebahatika kuingia THT kupata mafunzo kutoka kwa Barnaba. Alisema mshindi huyo pia atapelekwa Studio kurekodi nyimbo pamoja na kushirikiana kurekodi na Msanii nyota nchini Diamond. Aliongeza kuwa Siku ya Jumapili kuanzia majira ya saa nane mchana kutakuwa na Semina ya kutambua fursa ambapo hakuta kuwa na kiingilio na mtu yoyote anakaribishwa semina itakayofanyikia katika ukumbi wa Mkapa. Alisema kuanzia saa 12 jioni sherehe nzima zitahamia kwenye viwanja vya Sokoine hadi majogoo kwa kiingilio cha shilingi 5,000 kwa mtu mmoja. Akizungumzia kuhusu usalama wa Uwanja Hussein alisema wamejipanga kuimarisha ulinzi na kuhakikisha sehemu ya kuchezea mpira(PITCH) haiguswi kwa kuzungushiwa fensi. Alisema Serengeti Fiesta imeshafanyika katika viwanja vya Shinyanga naMorogoro sehemu ya kuchezea mpira haijaguswa kabisa hivyo wanauhakika wa kuulinda uwanja wa Sokoine usiharibiwe. Mwisho. Na Mbeya yetu |