Monday, September 15, 2014

MKUTANO WA USAJILI WA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI KUFANYIKA JIJINI DAR, SEPTEMBA 18



MKUTANO WA USAJILI WA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI KUFANYIKA JIJINI DAR, SEPTEMBA 18
Na Dotto Mwaibale 

 BODI ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi sasa imezifungia kampuni 36 na wakandarasi 86 kufanyakazi ya ukandarasi baada ya kushindwa kufuata sheria za ujenzi. 

 Hayo yalielezwa na Msajili wa bodi hiyo Jehad Jehad wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu mkutano wa usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi utakaofanyika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Septemba 18, 2014 jijini Dar es Salaam. 

 "Kazi yetu kubwa ni kusimamia sheria ya shughuli za ujenzi na kama tukibaini kuna kampuni inakwenda kinyume tunaifungia kufanyakazi" alisema Jehad. 

 Alisema lengo mkutano huo wa Septemba 18 ni kuwanoa wataalamu wa fani hiyo ili kukabiliana na mabadiliko ya kiteknologia na kitaaluma katika sekta ya ujenzi, kubadilishana mawazo na kuboresha huduma za taaluma hiyo. 

 Akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali Mwenyekiti wa bodi hiyo Dk.Ambwene Mwakyusa alisema Tanzania haina sheria inayoratibu shughuli za ujenzi kwa ujumla (Building Codes) itakayoweza kuwabana wajenzi ya maghorofa ambayo yanabomoka hapa nchini. Dk. Mwakyusa alisema sheria hiyo ingekuwepo ingewaongoza wataalamu wa majengo jinsi ya kutumia vifaa vya ujenzi kwenye jengo husika tofauti na ilivyosasa. 
Dk.Mwakyusa alisema kutokana na sheria hiyo kutokuwepo wataalamu wa majengo wanapotumia vifaa vya ujenzi ambavyo havina kiwango na wanapofikishwa kwenye vyombo vya sheria baada ya majengo wanayojenga kuanguka wanakutwa hawana hatia. 

"Tanzania haina sheria inayoratibu shughuli za ujenzi kwa ujumla kama ikiwepo sheria itamuongoza mtaalamu wa majengo afuate sheria iliyopo jinsi ya kutumia vifaa vya ujenzi mfano kama mbao au nondo zinatakiwa zitumike aina gani kwenye jengo husika ,"alisema Dk.Mwakyusa. Katika mkutano huo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaj Hassan Mwinyi.
  Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Dk.Ambwene Mwakyusa, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu mkutano huo. Kushoto ni Msajili Msaidizi Utawala na Fedha, Angello Ngalla na Msajili wa Bodi hiyo, Jehad A. Jehad.
 Msajili wa Bodi, Jehad A. Jehad (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Mkaguzi wa Ndani, Ezekiel Stephen na Kaimu Nsajili Msaidizi Ufundi, Mashaka Bundala.
 Kikao na waandishi wa habari kikiendelea.