……………………………………………………..
Na; Lucas Mboje
Kikao kazi cha Watendaji Wakuu wa Shirika la Magereza, Mfuko wa Jamii wa GEPF na Wataalam Washauri kimeendelea leo Agosti 1, 2014 Mkoani Morogoro. Lengo la Kikao hicho ni kupitia na kuangalia maeneo ambayo Uwekezaji katika mradi wa Majengo ya vitega uchumi utafanyika.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya mwanzo ya kuanza shughuli rasmi za ujenzi wa Majengo ya vitega uchumi kwa ubia kati ya Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Uzalishaji mali(Prisons Corporation Sole) na Mfuko wa Jamii wa GEPF.
Mpango huu wa ujenzi wa Majengo ya vitega uchumi unatarajiwa kuanza mapema mwishoni mwa Mwaka 2014 mara baada ya kukamilika kwa michoro na mahitaji mengine muhimu ambapo unatarajiwa kutekelezwa katika maeneo ya Jeshi la Magereza ya Kihonda Mkoani Morogoro na Karanga – Moshi Kilimanjaro.
Tayari, Jeshi la Magereza nchini kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali limetiliana Mkataba wa Uwekezaji wa Mfuko wa Jamii wa GEPF ambapo Majengo ya vitega uchumi yatajengwa katika maeneo ya Kihonda Mkoani Morogoro na Karanga – Moshi Mkoani Kilimanjaro. Utiwaji sahini ya Mkataba huo ulifanyika Mei 29, 2014 katika Ukumbi wa Mikutano ulioko Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Kupitia ubia huo Shirika la Magereza litapata pato ambalo litaimarisha zaidi upanuaji wa shughuli za miradi ya Shirika hilo sambamba na kuipunguzia gharama Serikali.
Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake tayari limefikia makubaliano na Wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ambao wamevutiwa na shughuli za kiuwekezaji kwa lengo la kuingia ubia hivyo kukuza mitaji na kubadilishana ujuzi katika miradi mbalimbali ikiwemo ya Madini na Kilimo katika maeneo ya Jeshi la Magereza.
Wakati huo huo, Jeshi la Magereza Tanzania Bara lipo katika maandalizi ya mwisho ya kuzindua TOVUTI yake ambapo kupitia Tovuti hiyo itarahisisha Mawasiliano pia Wananchi na Wadau mbalimbali watapata taarifa muhimu kuhusiana na Jeshi hilo. Tovuti hiyo itapatikana kupitia akaunti ya Anuani yawww.magereza.go.tz.