Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika kituo maalumu cha kulea watoto hao Buhangija Manispaa ya Shinyanga, wamezidi kuongezeka kituoni hapo kutokana na wimbi la mauaji ya albino kuibuka tena.
Hadi juzi kituo hicho kilifikishiwa watoto zaidi ya 100.
Pia watoto wengi wametoka kwenye mikoa ya Tabora, Simiyu na Mwanza.
Mei mwaka huu mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi aliuawa mkoani Simiyu na wengine wawili mkoani Tabora.
Taarifa iliyotolewa wakati wa hafla fupi ya kukabidhi misaada iliyopatikana kupitia harambee iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali Easy Flex la mjini Shinyanga kwa kituo hicho, imesema kwamba tangu mauaji hayo yaanze upya kila siku watoto watatu mpaka wanne wenye ulemavu wa ngozi wanapokelewa kituoni hapo.
Aidha watoto waliopata nafasi ya kuzungumza waliiomba serikali kusimamia kidete uhai wao.
Rehema Masunga, Mkama Shakengwa na Daniel Limbu wanaosoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Buhangija, walisema Tanzania inasifika kwa kuwa na amani lakini sasa hali inaelekea kuwa mbaya kutokana na baadhi ya watu kuwa na roho za kikatili na kuuwa binadamu kama wanyama .
"Inasikitisha sana kuibuka tena mauaji ya albino tuliona kwenye vyombo vya habari watu wamekatwa mkono, naiomba jamii iwapuuze waganga wa kienyeji maana ndiyo wanachangia, tumuamini Mungu atatuepusha na unyama huu wa kikatili," alisema Limbu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye pia ni msimamizi wa kituo, Peter Ajali, akizungumza kwenye hafla hiyo mbele ya Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Ghulam Hafidh aliitaka jamii kuwa na utamaduni wa kusaidia kituo hicho,badala ya kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili huku akisisitiza mikoa yote iliyopeleka watoto kutoa michango itakayosaidia kukidhi mahitaji na kuwaomba kuielimisha jamii umuhimu wa kusaidia.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Easy Flex, Happiness Kihama alisema changamoto kubwa iliyopo ni uelewa mdogo kwa jamii, juu ya kusaidia vituo hivyo vyenye mahitaji maalumu wazee na walemavu kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uchakavu wa majengo, chakula na malazi.