Thursday, August 28, 2014

Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya Nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa nchi za Afrika kufanyika Agosti 29, jijini Dar


mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya Nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa nchi za Afrika kufanyika Agosti 29, jijini Dar
Mheshimiwa Dk. Binilith Mahenge Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira ametoa rai kwa Wananchi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla kuweka juhudi katika kupambana na changamoto za mabadiliko ya Tabia Nchi.

Alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar-es-salaam kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na Mambo ya Nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika jijini Dar-es -salaam katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere Tarehe 29 Agosti 2014.

Alisema kuwa Tanzania imeandaa mkutano wa Mawaziri wa Mazingira na mambo ya nje kutoka nchi za kamati ya wakuu wa nchi za Afrika kuhusu tabia nchi lengo likiwa ni kutoa mwongozo wa namna ya kushughulikia changamoto na mabadikiko ya tabianchi na namna ambavyo nchi za Afrika zitavyoweza kunufaika na rasilimali zinazotolewa na nchi zilizoendelea ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

Mkutano huo ambao utakuwa ni mwendelezo wa juhudi za viongozi wa Afrika katika kushughulikia na kutoa mwongozo wa namna ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimeendelea kuliathiri Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Anasema kuwa joto la dunia limeongezeka kutokana na kuongezeka kwa gesi joto kama vile hewa ukaa ambayo inatokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji na matumizi ya nishati, viwanda na usafirishaji.

"Mabadiliko haya ya tabianchi yanaathiri zaidi watu ambao ni maskini zaidi na wengi ni wale waishio bara la Afrika.Hivyo basi nchi za Afrika zinahitaji rasilimali fedha za kutosha ili kukabiliana na madhara hayo ambayo yanatokana na Mabadiliko ya tabianchi" Alisema Dk.Mahenge.

Aliongeza kuwa mkutano huo utajadili zaidi mambo yanayoathiri kwa kiasi kikubwa Mazingira , hivyo utapendekeza masuala muhimu kwa bara la Afrika hasa upatikanaji wa fedha na tekinolojia katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko hayo barani Afrika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais –Mazingira Mh. Dk. Eng. Binilith Satano Mahenge (kushoto), akiwa pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya makamu wa Rais, Bwana Sazi Saula wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano utakaofanyika jijini Dar es Salaam Tarehe 29 Agosti 2014 .
Sehemu ya waandishi wa habari wakisikiliza hotuba inayotolewa na Mheshimiwa Dk. Eng. Binilith Satano Mahenge (hayupo pichani).