RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amezitaka jamii nyingi za kiafrika kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na mchango wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo nchini.
Mhe. Mkapa ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Jiolojia uliowakutanisha wataalam mbalimbali wa mambo ya jiolojia ulimwenguni akiwa ameongozana na Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu Waziri wake, Mhe. Stephen Masele.
Mhe. Mkapa ameeleza kuwa ni vema kwa wanasayansi ulimwenguni kujenga utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kujadili mambo yanayohusu sayansi na teknolojia ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii ambazo zitatatua migogoro inayoweza kujitokeza baina ya nchi na wawekezaji.
"Jamii nyingi za kiafrika hazijaelewa mchango mkubwa wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo lakini maendeleo daima yanatokana na rasilimaliwatu juu ya ardhi na chini ya ardhi, mchango wake huu hauthaminiwi na wengi lakini wanaoweza kufanya hivi ni wanasayansi". Alisema Mhe. Mkapa.
Aidha, Mhe. Mkapa ameishauri serikali licha ya kudhamini mafunzo mbalimbali na masomo kwa vijana nje na ndani ya nchi, fedha za kutosha bado zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakuwa endelevu.
Mhe. Mkapa ameongeza kwa kuwaasa vijana hasa vijana wa kike kujenga utamaduni wa kujikita katika masomo ya sayansi ili waweze kuwa wabunifu na kujikwamua na maisha yao.
Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini Wiliam Mkapa akiwahutubia wajumbe waliohudhuria mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma akitoa hotuba yake fupi mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Wajiolojia Afrika Profesa Aberra Mogessie akiwahutubia wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa, Sospeter Muhongo akitoa hotuba yake mbele ya wajumbe (hawako pichani) baadhi ya kazi mbalimbali alizowahi kuzifanya katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na mada Kuu ya Mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Baadhi wa wajumbe waliohudhuria mkutano wa Jiolojia wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini Wiliam Mkapa (wa pili toka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliohudhuria mkutano wa Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma, anayemfuatia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. Stephen Masele. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo. PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO.