Monday, August 25, 2014

‘MADINI HOUSE’ KUJENGWA ARUSHA, Kuwa na huduma za kibenki, Helkopita kutua moja kwa moja kituoni



'MADINI HOUSE' KUJENGWA ARUSHA, Kuwa na huduma za kibenki, Helkopita kutua moja kwa moja kituoni
Na Asteria Muhozya, Songea
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini itajenga kituo maalum cha kuuza na kununua madini ya vito kutokana na nchi kuwa na hazina kubwa ya madini jambo ambalo pia litachangia katika kuyaongezea thamani madini hayo. 
 Masanja ameyasema hayo  mjini Songea wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Eliakim Maswi kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara ikiwemo kuonana na Makamishna Wasaidizi wa Kanda, Maafisa Madini Wakaazi, Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania, kuangalia shughuli za wachimbaji wadogo wakiwemo wafanyabiashara wa madini na wawekezaji katika sekta ya madini. 
 Kamishna aliongeza kuwa, kituo hicho kitakuwa na huduma zote muhimu zikiwemo za kibenki ambazo zitawawezesha wachimbaji na wafanyabiashara kutokutafuta huduma muhimu zinazoendana na shughuli hizo nje ya kituo hicho. 
"Shughuli zote za uuuzaji na ununuzi madini ya vito na usonara zitafanywa katika kituo hicho. 
Kutakuwa pia na helkopita itakayotua moja kwa moja katika jengo hilo jambo ambalo litawezesha uwepo wa usalama katika biashara nzima ya kuuza na kununua madini," alisisitiza Masanja. 
 Aidha, aliongeza kuwa, ili kuiwezesha sekta hiyo kupaa kwa kasi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi, wizara imeamua kuanza kwa kuboresha ofisi za kanda za madini ikiwa ni pamoja na kununua maeneo maalum kwa ajili ya kujenga ofisi hizo ili kuboresha utendaji wa sekta ya madini nchini na kuwa na ofisi za uhakika. 
 "Tunataka kupitia sekta ya madini kuiwezesha serikali kuongeza mapato yake na kutoka hapa tulipo kiuchumi. Jambo hilo linawezekana ndio sababu tunaanza na kuboresha sehemu za kazi ili kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira mazuri zaidi na kuongeza uwajibikaji,"aliongeza Masanja. 
Katika hatua nyingine, Kamishna Masanja amewataka Makamishna Wasaidizi wa Kanda na Makamishna Wakaazi walioteuliwa hivi karibuni kutimiza wajibu wao vizuri na kufikia lengo la makusanyo ambayo wizara imewapangia na kwa wale wasiotekeleza agizo hilo la makusanyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu wataondolewa katika nafasi zao. 
"Tumeamua kupaa kupitia sekta hii, asiyeweza kutekeleza jambo hili kama tulivyokubaliana, tutamwondoa na kuwapa wengine wenye uwezo wa kufanya hivyo. Tunataka kufanya kazi kwa kasi na kisasa zaidi," alisisitiza Masanja. 
Wakati huo huo, aliwata watumishi wote walioko katika ofisi za Kanda kuwa waadilifu, wawajibikaji, wawazi na wabunifu ili kuweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwemo kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. 
Vilevile, aliongeza kuwa, wizara imejipanga kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki kuanzia mwezi Septemba kwa ajili ya waombaji wa leseni jambo ambalo litasaidia kurahisisha zoezi la uombaji wa leseni na kuondoa manungu'niko miongoni mwa waombaji.
Afisa Madini Mkaazi Tunduru Fredrick Mwanjisi (kushoto) akifurahia jambo wakati akimwongoza Katibu Mkuu Nishati na Madini Eliakim Maswi (wa pili kushoto) kutembelea eneo itakapojengwa ofisi ya Madini Tunduru. Wengine katika picha ni ujumbe wa Maafisa walioongozana na Katibu Mkuu na watumishi wa ofisi ya Madini Tunduru.
Jengo ambalo litatumika kama  Makao Makuu ya Ofisi ya Madini Kanda ya Ziwa Nyasa mjini Songea. Jengo hilo limenunuliwa na Wizara na litaanza kutumika mara baada ya ukarabati. Wengine katikati ni Kaimu MKurugenzi Idara ya Utawala Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Msika na wengine ni maafisa wWizara ya Nishati na Madini na Maafisa wa Madini Kanda waliofuatana na Katibu Mkuu.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja, (wa kwanza kushoto) akitafakari jambo mara baada ya kukagua kiwanja kitakapojengwa ofisi ya Madini ya Kamishna Mkaazi wa Madini, Nachingwea. Wa pili kushoto ni  Katibu Mkuu  Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kwanza, wengine ni  Afisa Madini Mkaazi Nachingwea, Mhandisi Mayigi Makolobela (wa pili kulia) na wa kwanza kulia ni Mjiolojia kutoka ofisi ya Madini Mtwara.