Ujumbe wa Tanzania uliopo nchini Canada kwa ziara ya mafunzo ukiongozwa na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga (aliyenyoosha mkono), ukiwa katika chumba cha kusimamia mitambo ya kuzalisha methano (haionekani pichani) katika kiwanda cha kuzalisha malighafi hiyo kilicho katika jimbo la Alberta nchini Canada.
Ujumbe wa Tanzania uliopo nchini Canada ukiongozwa na Naibu Waziri Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa nne kutoka kushoto, waliosimama), ukiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa kampuni ya kimataifa ya kuzalisha na kusafirisha methano ya nchini Canada mara baada ya kufanya ziara ya mafunzo katika kiwanda hicho. Wengine katika picha ni Naibu Waziri, TAMISEMI, Kassim Majaliwa, (wa nne kutoka kulia, waliosimama). Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Ummy Mwalimu, (wa pili kutoka kulia waliosimama) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Kampuni ya kimataifa inayotengeneza na kusafirisha malighafi methano ya nchini Canada 'Methanex' imeeleza Kuwa Tanzania ni moja ya maeneo muhimu duniani yanayofaa kwa uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza malighafi hiyo ambayo inatumika kuzalisha kemikali mbalimbali kutokana na uwepo wa hazina kubwa ya gesi asilia.
Hayo yamesemwa na Bw.Kevin Handerson, Makamu wa Rais wa kampuni ya Methanex kwa upande wa Amerika Kaskazini wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga uliofika katika kiwanda cha kuzalisha methano kilicho katika jimbo la Alberta nchini Canada ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo kuhusu usimamizi na uendelezaji wa tasnia ya uziduaji.
Bw.Handerson ameeleza kuwa uzalishaji wa methano utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kutokana na malighafi hiyo kutumika katika masuala mbalimbali ikiwemo kutengeneza vifaa vya plastiki, gesi inayotumika majumbani, kutumika kwenye vyombo vya usafiri, viwanda vya kutengeneza rangi, viwanda vya mbao, kuzalisha umeme, kusafishia maji n.k
" Pamoja na Tanzania Kuwa ni eneo muhimu kwa uwekezaji wa viwanda hivi vya kuzalisha methano ni muhimu Serikali ikatenga eneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa namna hii, na kuzingatia uwepo wa sera, sheria, kanuni madhubuti zinazoongoza sekta hii, pia kuwe na miundombinu imara ya usafirishaji, maji, umeme wa uhakika pamoja na uwepo wa rasilimali watu". Alisema Bw. Handerson
Akieleza kuhusu uwezo wa kampuni hiyo, Makamu Rais wa Methanex amesema kuwa, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha tani milioni 8.5 za methano kwa mwaka na husafirisha malighafi hiyo katika sehemu mbalimbali duniani ikiwamo Hongkong, Shanghai, Beijing, Seoul, Tokyo, na Brussels.
Vilevile Bw. Handerson ameeleza kuwa kampuni hiyo ya Methanex ipo tayari kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa wanauzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika uwekekezaji wa viwanda hivyo, wana mfumo mzuri wa kutoa mafunzo kwa wazawa ili kushiriki katika miradi ya methano, vilevile wako tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuendeleza rasilimali hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga aliikaribisha kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa kuna kiasi kikubwa cha gesi asilia cha zaidi ya futi za ujazo trilioni 50 ambacho pamoja na kutumika kuzalisha umeme pia inaweza kutumika kwa shughuli nyingine za kiuchumi ikiwamo kutengeneza methano na mbolea.
Alisema kuwa kuwa serikali ya Tanzania inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta za Nishati na Madini ili kuleta maendeleo endelevu ya sekta hizo na kwamba zipo sera, sheria na kanuni nzuri ambazo pamoja na mambo mengine zinalenga kuvutia uwekezaji katika tasnia hiyo.
Katika Ziara hiyo ya Mafunzo, Naibu Waziri Kitwanga ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ( TAMISEMI), Kassim Majaliwa.