Tuesday, July 22, 2014

SERIKALI YAHAHA KUMSAKA BALALI ALIYE HAI...



SERIKALI YAHAHA KUMSAKA BALALI ALIYE HAI...
Aliyekuwa Gavana wa Benki ya Tanzania  (BoT), Marehemu Daudi Balali enzi za uhai wake.

IKIWA ni takriban miaka sita sasa tangu aliyekuwa Gavana wa Benki ya Tanzania  (BoT), Daudi Balali , afariki dunia nchini Marekani, serikali imesema inamsaka kwa udi na uvumba Balali feki anayepotosha Wabongo kwa kujifanya yu hai na anaendelea na maisha nchini humo.
Akizungumza na paparazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI) Isaya Mngulu alisema kuwa mtu huyo anasakwa kwa kuwa anatenda kosa la jinai.

"Kutumia mtandao kujifanya wewe ni mtu fulani wakati siyo ni kosa la jinai, hivyo tunamtafuta ili achukuliwe hatia za kisheria," alisema DCI Mngulu.
Mngulu alikuwa akijibu maswali ya waandishi wetu waliofanya uchunguzi na kugundua kuwa kuna mtu anatumia mtandao wa Twitter kujifanya ni Balali na kukanusha kuwa hajafariki dunia.
paparazi walitaka kujua kwa DCI  hatua za serikali kwa mtu huyo ambaye huwa anaandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa aliwahi kuonana na Rais Jakaya Kikwete  nchini Marekani na kufanya mazungumzo.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai nchini (DCI) Isaya Mngulu.
Mtu huyo hakuishia hapo kwani hata hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilipochapisha kaburi la Balali lililopo Washington DC aliibuka na kukanusha kuwa yeye hajafa na kuzikwa.

"Naomba hizo nakala zake za alivyotwit ili tuzifanyie kazi," alisema DCI Mngulu baada ya kuoneshwa nakala za maelezo ya Balali feki kwenye mtandao.
DCI alipewa nakala hizo na waandishi wetu na kuahidi kumsaka mtu huyo.
Naye Afisa wa Mawasiliano Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), Semu Mwakyanjala alipofuatwa ofisini kwake na waandishi wetu na kuelezwa kuhusiana na Balali huyo feki alisema anachokifanya mtu huyo ni kitendo cha kihalifu.
"Ukweli ni huo kwamba anatenda uhalifu na polisi watakapohitaji mambo ya kitaalamu kuhusiana na suala hilo tutatoa ushirikiano ili mtu huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria," alisema Mwakyanjala.
Balali, alifariki dunia Mei 16, 2008 huko Boston, nchini Marekani, wakati ambao alikuwa akiaminika kuwa shahidi muhimu wa kashfa ya wizi wa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Tangu wakati huo hadi sasa tunapoandika habari ya Balali feki, kumekuwa na kauli zinazoashiria kuwapo hali ya kutiliwa shaka kuhusu ukweli wa kifo chake, na bila shaka mtu huyo anayejifanya ni Balali anaitesa na kuikasirisha familia yake.