Saturday, July 19, 2014

Samatta Aaga Team ya Mazembe, Sasa Kucheza Ulaya


Samatta Aaga Team ya Mazembe, Sasa Kucheza Ulaya
ANAONDOKA! Ndiyo, unaweza kusema hivyo kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyemuaga tajiri wa timu hiyo, Moisse Katumbi Chapwe, kwenda kukipiga barani Ulaya na amekubaliana na uamuzi wake.

Samatta amekuwa akidaiwa kunyemelewa na baadhi ya timu kutoka mataifa ya Ulaya kama vile Ufaransa, Ureno, Urusi na Ubelgiji, kutokana na kipaji kikubwa anachokionyesha cha kusakata kabumbu.

Samatta aliliambia Udaku kwa njia ya mtandao kutoka nchini Tunisia ilipoweka kambi Mazembe kuwa ndani ya miaka miwili ijayo amepanga kucheza soka kwenye ligi kubwa barani Ulaya na tayari ameshazungumza na Katumbi juu ya suala hilo na amekubaliana naye.

"Nimepanga ndani ya miaka miwili ijayo nicheze kwenye ligi kubwa ulimwenguni, nimezungumza na bosi wa timu, Katumbi kaniruhusu na kuniambia suala hilo halina tatizo, pia amesema ataniachia na hawatanibania timu ikija kunisajili," alisema Samatta.

Katika hatua nyingine, Samatta alisema timu yao imeshindwa kuweka kambi barani Ulaya kwenye nchi ya Ubelgiji kutokana na baadhi ya wachezaji kukosa viza ya kuingilia nchini humo. Kwa sasa wapo nchini Tunisia wakijiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.

Kwa miaka mingi sasa Mazembe imekuwa ikidaiwa kuwabania nyota wake kujiunga na timu za Ulaya kwa lengo la kujiimarisha, lakini msimu uliopita ilimuuza nahodha wake, Tresor Mputu, kwenda timu ya Kabuscorp ya Angola aliyokuwa akichezea Mbrazil, Rivaldo,

Mazembe pia imemuuza beki raia wa Zambia, Stopilla Sunzu, aliyesajiliwa na Sochaux ya Ufaransa inayonolewa na kocha wa zamani wa Zambia, Herve Renard.

Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 akitokea timu ya Simba, iliyomuuza kwa dau la Dola za Kimarekani 100,000 (sawa na Sh. milioni 150 za Tanzania za wakati huo), huku yeye mwenyewe akipewa Dola za Kimarekani 50,000 za usajili.