Wednesday, July 02, 2014

Mukabwa aitwa Kuvua Viatu Mashabiki


Mukabwa aitwa Kuvua Viatu Mashabiki
 
Waimbaji nyota wa muzki wa Injili,Anastazia Mukabwa akiwa amepozi na Rose Muhando.

MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili nchini Kenya, Anastazia Mukabwa, ni miongoni mwa wakali ambao mwimbaji Rose Muhando anatamani wawepo kwenye uzinduzi wa albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu.
 
Rose Muhando amepanga kuzindua albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu Agosti 3, mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.
 
Akizungumza na gazeti hili, Muhando alisema Mukabwa aliyemshirikisha katika wimbo wa Vua Kiatu ni aina ya wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuimba na kwamba tayari ameiomba Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wake iwasiliane na msanii huyo kuhakikisha anapatikana siku hiyo.
 
"Wapo waimbaji wengi wa Injili natamani wawepo siku hiyo, lakini ningefurahi kama ningempata Anastazia Mukabwa wa Kenya, hivyo tayari nimeiomba Kamati ya Maandalizi ifanye kila iwezalo aje.
 
"Ni aina ya uzinduzi wa pekee ambao nataka ufanyike siku hiyo, ni imani yangu tutampata Mukabwa na wakali wengine," alisema na kuongeza kuwa ujio wa Mukabwa utakuwa mzuri ili mashabiki 'wavue viatu' siku hiyo.

Nyimbo zilizopo katika albamu ya Kamata Pindo la Yesu ni Bwana Niongoze, Wewe Waweza, Usiniache, Nibariki, Muongo, Kwema, Kamata Pindo la Yesu na Facebook.


Hivi sasa Rose anatamba na albamu yake ya Utamu wa Yesu yenye nyimbo saba, ambapo albamu zake nyingine ni Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange Sawasawa, Kitimutimu, Mungu Anacheka na Wololo.