Tuesday, July 22, 2014

MARCIO MAXIMO MAJARIBUNI KOMBE LA KAGAME 2014, CECAFA YAANIKA MUZIKI WA YANGA SC




MARCIO MAXIMO MAJARIBUNI KOMBE LA KAGAME 2014, CECAFA YAANIKA MUZIKI WA YANGA SC
KUMEKUCHA! Ndivyo unaweza kusema!. Baraza la vyama vya soka kwa ukanda wa Afrika mashariki na kati, CECAFA limetoa ratiba ya michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati,maarufu kwa jina la `Kagame Cup` itakayofanyika mwaka huu, mjini Kigali nchini Rwanda kuanzia Agost 8.Mabingwa wa Tanzania msimu wa 2012/2013, Dar Young Africans wataanza kampeni ya kusaka taji hilo Agosti 8 mwaka huu dhidi ya Rayon katika dimba la  Amahoro mjini Kigali.Hii itakuwa mechi ya kwanza ya mashindano kwa kocha mkuu wa Wanajangwani, Mbrazil Marcio Maximo aliyetua Yanga mwaka huu baada ya Mholanzi Hans van Pluijm kumaliza mkataba wake na kutimkia Saudi Arabia sambamba na aliyekuwa msaidizi wake Charles Boniface Mkwasa `Master`. 
Andrey Coutinho (kushoto) akipasha moto misuli

Pia wachezaji wawili raia wa Brazil, Gleison Santos Santana na Andrey Coutinho watacheza mechi yao ya kwanza siku hiyo wakiwa kwenye uzi wa njano au kijani.
Mechi nyingine siku ya ufunguzi itawakutanisha Atlabara dhidi ya KMKM ya Zanzibar kwenye uwanja wa Nyamirambo, wakati Gor Mahia ya Kenya itacheza dhidi ya KCCA.
Agosti 10 mwaka huu, Yanga watacheza mechi ya pili ya kundi A dhidi ya Watanzania wenzao, KMKM ya Zanzibar. Na Agosti 12 mwaka huu Maximo ataiongoza tena Yanga kupepetana na Atlabara.
Agosti 16 Yanga itaoneshana kazi na Coffee katika mchezo wa mwisho wa kundi A.
Robo fainali ya kombe la Kagame itaanza kutimua vumbi Agosti 19 mwaka huu.
Afisa habari wa CECAFA , Rogers Mulindwa katika taarifa yake mchana huu amesema muda wa kuanza kwa mechi utapangwa kwa makubaliano kati ya CECAFA, shirikisho la soka nchini Rwanda (FERWAFA) na kituo cha luninga cha Supersport ambacho kitarusha moja kwa moja michuano hiyo.
Michuano ya Kagame ndio sababu kubwa ya shirikisho la soka Tanzania TFF,  kusogeza mbele michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara hadi septemba 20 mwaka huu kwa lengo la  kuwasubiri Yanga.
Awali ligi kuu ilitakiwa kuanza kushika kasi Agosti 24 mwaka huu, lakini kutokana na sababu tofauti kubwa ikiwa ni hiyo ya Kagame, ratiba akapigwa teke.
Yanga kwasasa wanaendelea na mazoezi ya kujiweka fiti kuelekea katika michuano hiyo katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola.
Kocha Maximo alisema ataitumia michuano ya Kagame kuona kikosi chake ili kujua mapungufu yako wapi na kuyarekebisha kabla ya kuanza ligi kuu.
Hata hivyo wachezaji wa Yanga waliopo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinachojiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Msumbuji wiki mbili zijazo, hawapo kwenye Mazoezi hayo.
Wachezaji walipo Taifa stars ni Deogratius Munish `Dida`, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Haroub `Cannavaro`, Saimon Msuva na Mrisho Khalfani Ngassa.
Pia nyota wake wa kimataifa, Emmanuel Okwi, Khamis Kiiza `Diego` (Uganda) na Haruna Niyonzima (Rwanda) wapo  katika majukumu ya timu zao za taifa katika michuano ya mtoana kusaka tiketi ya kucheza michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, AFCON mwakani nchini Morroco.