Na Othman Khamis Ame, OMPR
Wakati kumi la mwanzo la Rehema na lile la pili la maghfira yaliyomo ndani ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan yakimalizika waumini wa Dini ya Kiislamu hivi sasa wanaendelea na ibada katika kukamilisha kumi la mwisho la mwezi huu mtukufu wa Ramadhani la kuachwa huru na moto.
Ibada hii ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani inamuwajibikia kila muumini wa Dini hiyo aliyefikia balegh na akili timamu kuitekeleza ikiwa ni ya Nne kati ya tano ya nguzo za Kiislamu.
Harakati za kufutari pamoja kama ibada miongoni mwa waumini hao zimekuwa zikiendelea kushamiri katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja ,Pemba, Tanzania na Mwambao mzima wa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Hali hiyo ikajitokeza katika Kijiji cha kidoti kiliopo Wilaya ya Kaskazini " A" Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo wanafunzi wa Madrasatul Hidayatul Islamia ya Kijiji hicho ikajumuika na baadhi ya wazazi, walezi na viongozi wa Serikali na Siasa wa eneo hilo katika kufutari pamoja.
Mjumuiko huo unaojenga imani na mapenzi umeongozwa na Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziubar Mama Asha Suleimani Iddi akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini " A " Bibi Riziki Juma Simai.
Utamaduni wa kufutari kwa pamoja miongoni mwa waumini wa dini ya Kiislamu umekuwa ukizidi kushamiri kila pembe ya visiwa hivi zikionekana kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Taasisi mbali mbali za Umma, Binafsi na hata zile za kiraia.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mama Asha Suleiman Iddi akijumuika pamoja na wana Madrasa ya Hidayatul Islamia ya Kidoti hawapo pichani kwenye futari ya pamoja ndani ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Kulia ya Mama Asha ni Mkuu wa Wilay ya Kaskazini " A " Bibi Riziki Juma Simai na Kushoto yake ni Katibu wa Mardasa hiyo Bi. Ukti Dawa Vuai.
Baadhi ya Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Madrasatul Ismalia ya Kijiji cha Kidoti wakijumika na watoto wao katika futari ya pamoja iliyojumisha pia viongozi wa Serikali na Kisiasa wa Wilaya ya Kaskazini " A ".
Mama Asha Suleiman Iddi akibadilishana mawazo na Katibu wa Madrasatul Islamia ya Kidoti Bi. Ukti Dawa Vuai kabla ya futari ya pamoja iliyofanyika kwenye Mdrasa hiyo hapo Kidoti.
Mama Asha akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini " A " kulia yake Bibi Riziki Juma Simai akiwashukuru wakaazi wa Kijiji cha Kidoti pamoja na Wanafunzi wa Madrasatul Islamia mara baada ya kufutari nao pamoja Chuoni hapo.
Mama Asha akiaga rasmi wakaazi wa Kijiji cha Kidoti mara baada ya kukamilika kwa futari ya pamoja iliyojumuisha wazazi, walezi na baadhi ya wakaazi wa kijiji hicho. Picha na Hassan Issa wa OMPR