Wednesday, July 02, 2014

Kisomo cha 40 ya Marehemu Amina Ngaluma kufanyika Jumamosi jijini Dar



Kisomo cha 40 ya Marehemu Amina Ngaluma kufanyika Jumamosi jijini Dar
Na Mwandishi Wetu

KISOMO cha 40 ya aliyekuwa mwimbaji mahiri nchini, marehemu Amina Ngaluma 'Japanese' kinatarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Kitunda, Machimbo Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, mume wa marehemu Rashid Sumuni, alisema kisomo hicho kitafanyika nyumbani kwa wazazi wake marehmu na kwamba pia watakuwa na shughuli maalum ya kufutarisha waumini baada ya kumalizika kisomo hicho.

"Tunaomba ndugu, jamaa na marafiki wote tulioshiriki kwa namna mbalimbali wakati wa msiba wa marehemu mke wangu, tushirikiane pia katika 40  siku hiyo," alisema Sumuni na kueleza kuwa shughuli hiyo itaanza baada ya swala ya alasiri.

"Naomba wanamuziki wenzangu, mashabiki wake, pamoja na wadau wengine wa muziki na marafiki wote, tushirikiane katika tukio hili na tutakapomaliza kusoma, tutafuturu pamoja nyumbani kwa wazazi pale pale Machimbo," alisema Sumuni.

Ngaluma aliyepata kung'ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Mei 15 mwaka huu kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor na kuzikwa Mei 24 jijini Dar es Salaam.

Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution 'Tamtam',  Double M Sound 'Mshikemshike' na TOT Plus zote za Dar es Salaam.

Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.

Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize.

Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili,  Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma 'Kocha wa Dunia'.