WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amenusurika kifo hivi karibuni baada ya ndege ya shirika la Precision Air, iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kupata hitilafu ya injini.
Ndege hiyo, ambayo iliondoka Mwanza saa 2:30 usiku, ilipata hitilafu ya injini moja muda mfupi tu baada ya kuruka, hali iliyomlazimu rubani wa ndege hiyo kubadili mwelekeo na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akizungumza na Mtanzania jana, Sumaye, ambaye alikuwa mmoja wa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Sumaye alisema kitendo cha injini kupata hitilafu, ilimlazimu rubani wa ndege hiyo kuruka na injini moja mpaka KIA, ambako walitafutiwa ndege nyingine ili kuendelea na safari.
Alisema kutokana na tatizo hilo, abiria walilazimika kuondoka KIA kwa kugawanywa kwenye ndege tofauti zilizokuwa zikielekea Dar es Salaam ambapo Sumaye aliondoka saa 7 kasoro usiku.
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bestina Magutu, alipotafutwa ili kujua kilichotokea kwenye ndege hiyo, alisema kuwa hakuwa na taarifa zozote za hitilafu ya ndege hiyo.
"Hebu ongea nao wenyewe, sijapata taarifa zozote mpaka sasa, nimetoka ofisini jana sikuwa na taarifa," alisema Magutu.
Naye Mratibu wa Masoko wa Precision Air, Hilaly Mremi, alipozungumza na Mtanzania alikiri kutokea kwa hitilafu hiyo ya ndege.
"Kwa kifupi hakuna ajali iliyotokea, hitilafu zinazotokea kwenye ndege ni za kawaida kama ambavyo gari inaweza kuharibika na kupakiwa pembeni," alisema Mremi.
Alisema safari za shirika hilo zinaendelea kama kawaida na kutaja namba ya ndege hiyo kuwa ni TW 415.
Ndani ya wiki hii, ndege mbili za shirika hilo zimenusurika ajali baada ya kupata hitilafu wakati zikiwa angani.
Mbali na ndege hiyo aliyokuwemo Sumaye, ndege nyingine ya shirika hilo yenye namba ya safari Pw 77 na ya usajili TWC, iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda Kilimanjaro ilinusurika kupata ajali juzi jioni na hivyo kulazimika kurudi na kutua kwa dharura uwanjani hapo baada ya kupata hitilafu ikiwa angani.
Mbali na Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, naye aliwahi pia kupata ajali mwaka jana akiwa kwenye ndege za shirika hilo.
Lowassa alikuwa miongoni mwa abiria 37 waliokuwa wamesafiri na ndege hiyo ambayo ilipasuka magurudumu manne ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Katika ndege hiyo pia kulikuwa na maofisa mbalimbali wa Serikali na Jeshi la Wananchi, ambao walikwenda kuhudhuria sherehe ya kutolewa kamisheni kwa maofisa wa jeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA).