Watu wenye silaha wameua watu saba wakiwemo maafisa wanne wa polisi baada ya kushambulia basi la abiria katika kaunti ya Lamu kwenye mwambao wa Kenya.
Watu hao walishambulia basi hilo kwa risasi karibu na mji wa Witu, takriban kilomita 50 kutoka Lamu.
Baadaye walishambulia gari la polisi lililofika katika eneo la tukio.
Kundi la al-Shabab limesema limefanya shambulio hilo.
Basi hilo lililoshambuliwa siku ya Ijumaa lilikuwa likisafiri kutoka Mombasa kwenda Lamu. Watu hao walishambulia basi hilo baada ya kuziba njia na gari lao.
Dereva wa basi ni miongoni mwa waliouawa, amesema kamishna Miiri Njenga wa kaunti ya Lamu akizungumza na shirika la habari la Reuters.
Watu wanane wamelazwa hospitali, wengi kwa majeraha ya risasi.
Shambulio hili limekuja siku moja baada ya jeshi la Kenya kusema ndege yake imeteketeza kambi zinazotumika na kundi hilo katika eneo hilo.
Msemaji Wa al-Shabab, Abdulaziz Abu Musab, ameiambia Reuters kuwa tangazo hilo la Kenya ni "propaganda".
Kuhusu shambulio la Ijumaa, amesema ni "kujibu madai ya Kenya kuwa imepeleka wanajeshi wengi katika eneo la pwani na kuimarisha usalama".
Mamia ya familia zimekimbia makazi yao katika maeneo hayo kutokana na kutetereka kwa hali ya usalama ambayo pia imeathiri sekta ya utalii.