Ijumaa hii fursa imekuja; na hakika huu ndo wakati wake, maana 'Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.' Mhubiri 3:1 imeandika. Basi kwa wewe ambaye unajua ya kwamba una kipawa cha uimbaji, zoezi liko mbele yako ambalo litakufanya uingie studio za uhakika za Habari Maalum, kurekodi.
Na hapa unachotakiwa kufanya ni kuimba wimbo wa Tenzi; Cha Kutumaini Sina. Ni wewe tu na ubunifu wako ndio utakaokupeleka hatua nyingine katika uimbaji wako. Ni tarehe 18 kuamkia 19 kwenye mkesha wa vijana, FIREPLACE - HFCC, mwenyeji wa tukio akiwa Mchungaji Barnabas Philip. Pamoja naye watakuwepo walimu kwenye masuala ya uimbaji, Misericordias Anael pamoja na Peter Abednego.
Mkesha huo uliopewa jina la Worship Again, utakutanisha vikundi mbalimbali vya uimbaji kutoka maeneo tofauti kwa ajili ya BWANA kujitwalia utukufu. Tukutane kuanzia saa mbili usiku hadi kuku watakapokuwa wamefunguliwa banda, asubuhi.