Monday, June 30, 2014

ZITTO KABWE: FEDHA ZA IPTL NI MALI YA UMMA!




ZITTO KABWE: FEDHA ZA IPTL NI MALI YA UMMA!
Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika 'Tegeta Escrow Account' si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).

Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya 'Tegeta escrow' ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo kwa kushirikiana na 'mwekezaji' aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma. Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa 'Tegeta Escrow'.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya 'Tegeta Escrow'. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya 'Escrow'. Hata hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za 'Tegeta Escrow' zipewe kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).
Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.
Fedha zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250, katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012 kifungu cha 29).
Ni nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa 'Mnazi Bay North', jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali nyadhifa zao serikalini.
Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli ya Maswi kwamba "wanaume" hawazungumzi ndani ya Bunge si tu udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze kusimamia utaifa.