Na Richard                Bagolele-Chato.
        Wafugaji wa Ngo'ombe                Wilayani Chato mkoani Geita wameaswa kuachana na ufugaji                wa mazoea na badala yake wafuge kisasa zaidi.
        Wito huo umetolewa leo                Wilayani hapa na Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Rodrick                Mpogolo wakati akifungua  kikao cha pamoja na wafugaji wa                Ng'ombe na wataalam wa mifugo ambacho pia kilidhuriwa na                mwekezaji wa kiwanda cha kusindika nyama kutoka jijini                Mwanza cha Chobo Investiment.
        Mkuu wa Wilaya ya Chato                amesema wafugaji wengi nchini wamekuwa wakufuga Ng'ombe                wengi pasipo kupata mafanikio yoyote maishani jambo ambalo                amelikemea na kuwataka wafugaji kufuga  mifugo kidogo kwa                njia ya kisasa zaidi ambapo mafanikio yataonekana, " tuwe                na program za kumwendeleza mfugaji, mpango wa kufuga                mifugo wachache wenye tija badala ya kuwa na kundi kubwa                la Ng'ombe linaloongeza migogoro kila kukicha, tunataka                mifugo iwasaidie wafugaji kujiongezea kipato, kusomesha                watoto, kuwa na malazi mazuri na maisha bora kwa ujumla"                alisistiza Mkuu wa Wilaya.
        Katika hatua nyingine                mwakilishi wa kampuni ya uwekezaji ya Chobo Investiment                kutoka Mwanza Bw. Denis Kisoka amewahakikishia wafugaji                wilayani chato uwepo wa soko la uhakika wa Ng'ombe                waliofugwa kisasa ambapo hadi sasa amesema nyama                inayozalishwa nchini Tanzania bado haijakidhi vigezo                kutokana na ufugaji wa mazoea na hivyo kufanya kampuni                yake kushindwa kuzalisha nyama inayokidhi soko hasa kwa                baadhi ya wawekezajia wa kigeni waliopo hapa nchini.
        Amesema kampuni ya Chobo                Investiment wako tayari kutoa elimu kwa vikundi vya                wafugaji vilivyoko wilayani Chato ili waweze kuzalisha                mifugo bora na kukidhi mahitaji ya soko la nyama ambapo                kipato cha mfugaji pia kitaongezeka.
        Nao baadhi ya Wafugaji                waliochangia kwenye kikao hicho wameitaka serikali                kuboresha miundombinu kwa wafugaji hasa upatikanaji wa                majosho na elimu ya ufugaji wa kisasa. Wafugaji hao                wamesema uwepo wa maduka mengi ya dawa za mifugo                husababisha miundombinu inayojengwa na serikali                kutokutumika kutokana na wataalamu wa mifugo kujihusisha                na biashara hiyo.
        Bw. Noel Shadrack                mfugaji toka kijiji cha Buzirayombo amesema wafugaji                wakiamua kufuga kisasa wanaweza kwani ameshuhudia kwenye                baadhi ya minada ya Ngo'mbe hapa Wilayani Chato wakiuzwa                kwa shilingi 1,000,000 hadi 1,500,000 tofauti na bei ndogo                zilizozoeleka za shilingi 150,000 hadi 300,000.
        Nao baadhi ya watalaamu                wa mifugo wilayani Chato wamewalaumu baadhi ya wafugaji                kwa kufuga kwa mazoea na kuongeza kuwa baadhi ya wafugaji                hawako tayari kupokea ushauri wa wataalamu eti tu kwa                sababu wataalamu hao hawafugi chochote.
        Wamesema kutokana na                wilaya kutokuwa na maeneo makubwa ya malisho ya wanyama ni                vyema wafugaji hasa wa Ngo'ombe wakafuga kidogo ili                kukabiliana na tatizo hilo.
        Kikao hicho cha siku                moja kilikuwa na lengo la kumtambulisha mwekezaji wa                usindikaji wa nyama kutoka Mwanza Chobo Investiment                kimemalizika na kutoka na maazimio ya kuunda vikundi vya                wafugaji kutoka vijijini ili waweze kupata elimu ya                ufugaji bora na wa kisasa.
        Wilaya ya Chato                inakadiriwa kuwa na Ng'ombe wa asili zaidi ya 115,000                ambapo ufugaji huria umekuwa ukitumika katika maeneo yote                wilayani hapa.
                Mkuu wa Wilaya ya Chato                Mhe. Rodrick Mpogolo akiongea na wafugaji na wataalamu wa                mifugo kutoka Chato 
                wafugaji na wataalamu wa                mifugo wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato wakati                akifungua kikao hicho. 
        

 
