Na Mwene Said wa Globu ya Jamii
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, imeambiwa kwamba upelelezi wa kesi ya ubakaji inayomkabili Msanii Emmanuel Mbasha (32) - pichani - na mume wa Mwimbaji wa Injili, Flora Mbasha, umekamilika.
Hatua hiyo imefikiwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mh. Wilberforce Luago aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana na kwamba upelelezi wake umekamilika.
"Mheshimiwa kwa kuwa upelelezi wa kesi hii umekamilika tunaomba tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali…" alidai Katuga.
Hakimu Luago alisema mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali Julai 17, mwaka huu. Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo mshtakiwa alitimiza masharti ya mahakama na yuko nje kwa dhamana.
Katika kesi ya msingi, ilidai katika shitaka la kwanza kuwa, Mei 23, mwaka huu eneo la Tabata Kimanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria huku akijua ni kosa alimuingilia kwa nguvu msichana anayedaiwa kuwa shemeji yake (jina limehifadhiwa).
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 25, mwaka huu eneo la Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa aliumuingilia kwa nguvu mfanyakazi wake (jina limehifadhiwa).
Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashitaka hayo .
Awali, mahakama hiyo ilimtaka msanii huyo kuwa na wadhamini wawili, mmoja awe mtumishi wa serikali na mwingine kutoka taasisi inayotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 5.