Waandishi wa Habari kutoka mkoani Katavi wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Tume na Waandishi hao.
Na Kibada Kibada-Mpanda Katavi.
Imeelezwa kuwa Watanzania hawaoni thamani ya kupiga kura kwa sababu hata siku moja hawajawahi kunyimwa nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia.
Akifungua Mkutano wa siku moja wa waandishi Habari na Tume ya Taifa ya Uchaguzi unaohusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza na matumizi ya Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration uliofanyika Mjini Mpanda Mkoani Katavi, Mjumbe wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Prof.Amon Chaligha amesema watanzania walio wengi hawaoni thamani ya kupiga kura, hivyo vyombo vya Habari vinao wajibu Mkubwa wa kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura unatarajia kufanyika mwezi septemba mwaka huu kwa maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa Madiwani ,wabunge na Rais wa Jamhuri wa Tanzania mwezi oktoba mwaka 2015.
Akifafanua zaidi alisema Mataifa mengine ambayo raia wake walinyimwa uhuru wa kupiga kura, wao wanaona thamani kubwa sana ya kupiga kura, na ndio maana wanajitokeza kwa wingi katika kupiga kura kwenye chaguzi zao.
Akizungumzia maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia Teknolojia ya Biometrik Voter Registration amesema hii ni awamu ya kwanza ya mfumo huo wa BVR, hivyo watu wajitokeze kujiandikisha kwa kutumia mfumo huo mpya.
Awali Kamishina wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Gregory Kaijage amesema Tume inatarajia kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu.
Amesema demokrasia inasema kila mtu ana haki ya kupiga kura kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za uongozi unaokuwa ukifanyika kwa kufuata utaratibu kwa mujibu wa sheria za nchi..
Akiwasilisha mada inayohusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Vote Registration (BVR) ameeleza kuwa Tume inatarajia kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza hivi karibuni na maandalizi yake tayari yamekamilika kwa sehemu kubwa.
Akifafanua zaidi amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchanguzi imepewa jukumu la kisheria kuandikisha wapiga kura na kuboresha Daftari la hilo kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri wa Tanzania.
Akizungumzia matumizi ya biometric katika zoezi la uandikishaji , amesema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuingia katika mfumo huu wa BVR kwani tayari umekwishatumika katika nchi mbalimbali zikiwemo za kiafrika ingawa alieleza mafanikio hayo yaliambatana na changamaoto mabalimbali za kiteknolojia na kimfumo.
Alizitaja baadhi ya nchi za kiafrika zilizokwisha tumia mfumo huo kuwa ni pamoja na Nigeria 2007,Ghana 2009,Liberia2005,Guinea 2005,Mali2005,Uganda 2008,Kenya 20013,Zambia2008Afrika Kusini na Zanzibar 2009 na Tanzania itatumia mfumo huu katika uandikishaji wa wapiga kura tu.