Friday, June 20, 2014

STAMICO YAAHIDI NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI



STAMICO YAAHIDI NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI
1Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa wakiwa katika picha ya pamoja kwenye banda lao.
....................................................................................
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurungenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Madini la Taifa, Mhandisi Edwin Ngoyani ameahidi neema kwa wachimbaji wadogo wa madini na vito nchini kwa kuwawezesha kupata masoko ya bidhaa zao pamoja na kuwapatia zana za kisasa za uchimbaji madini.
"Malengo yangu makuu katika shirika hili ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanawezeshwa kunufaika na rasilimali za nchi yetu pamoja na kuhakikisha kwamba STAMICO linatoa mchango wa mapato katika mfuko mkuu wa hazina kwa kujiendesha kwa faida," Mhandisi Ngonyani alisema katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa kujiamini, Mhandisi Ngonyani alisema anatarajiwa malengo yake katika STAMICO yataanza kuzaa matunda ndani ya miaka miwili mpaka mitatu ijayo.
Akizungumzia mkakati kwa wachimbaji wadogo, Ngonyani alisema,ndani ya miaka miwili ijayo, shirika hilo litanunua mitambo miwili ya uchimbaji wa madini ya kisasa (drilling rigs) ambayo itatumiwa na wachimbaji wadogo.
"Lengo ni kuwafanya wachimbaji wadogo wanufaike na wawe sehemu ya uwekezaji kwenye rasilimali zao, kama ambavyo hao wawekezaji wa nje wanavyowekeza, na sasa watanzania nao watawekeza, ila lazima tuwawezeshe," Ngonyani alisisitiza.
Alisema lengo la STAMICO kwa wachimbaji wadogo ni kuhakikisha wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba kisasa ili pia watoa mitaji ambao ni benki wawe na uhakika wa fedha zao kurejeshwa, na kwamba hata ikibidi, shirika hilo litawawekea dhamana ili wawezeshwe kibenki.
Alisema hilo litawezekana baada ya mkakati wao wa kuanzisha na kuboresha takwimu za wachimbaji wadogo ambazo zitakuwa na taarifa zao ikiainisha mahali walipo,aina ya madini wanayochimba na mahitaji yao.
Pia mkakati mwingine ni kubaini vyanzo vya migogoro kwenye maeneo ya wachimbaji na kutafuta suluhu ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Katika hatua nyingine, Ngonyani alizungumzia mradi wa uchimbaji madini kwenye mgodi dhahabu wa Tulawaka ambao hivi sasa umenunuliwa na shirika hilo na kuitwa Biharamulo unaosimaimamiwa na kampuni ya StamiGold.
Alifafanua kwamba mgodi huo utaanza kazi rasmi Agosti 8, mwaka huu na kwamba baada ya miaka miwili na nusu, wanatarajia kupata faida ya shilingi bilioni saba.
Awali mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) na mwishoni mwa mwaka jana STAMICO ikaununua kwa dola za Marekani milioni tano.
ABG iliuza mgodi huo kutokana na kwamba kiasi cha wakia 100,000 kilichopo katika eneo la mradi ni kidogo kwa uchimbaji mkubwa kwa kampuni hiyo kubwa ya madini duniani.
"Hata hivyo tuna matumaini kwamba katika eneo la kilometa nne kutoka kwenye eneo la mradi kuna uwezekano wa kuwapo mashapo ya kati 150,000 mpaka 200,000. Tutaendelea na utafiti katika eneo hili," Mhandisi Ngonyani alisema.
Kwa upande wake, Meneja Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagweleka alisema hivi sasa miradi mitano iko kwenye ubia na shirika hilo kwa ajili ya uwekezaji na kuitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa Itetemia mgodi wa dhahabu ambao Stamiko wameingia ubia na Kampuni ya Madini ya Tancan Ltd.
Mradi mwingine ni wa Buckreef wa dhahabu ulioko Geita ambao Stamico wameingia ubia na Kampuni tanzu ya TANZAM 2000, ambapo Stamico wana hisa asilimia 45 na 55 iko kwa kampuni hiyo na kwamba wanategemea uzajishaji utaanza Novemba mwama huu.
Aidha mradi mwingine ni Kiwira ambao unazalisha makaa ya mawe kwa ajili ya kufua umeme utakaounganishwa kwenye gridi ya taifa.
Akizungumzia mradi huo,Meneja fedha na Utawala wa Stamico, Peter Gembe alisema lengo la mradi huo ni kufua megawati 200 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya taifa kutoka kwa kiwango cha awali cha megawati 6.
Stamico ni shirika la umma lililoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya madni katika pato la taifa na kuzalisha nafasi za ajira kwa watanzania.