Serikali imempa wiki tatu mkandarasi anayetengeneza barabara ya kilomita tatu ya kuingia makao makuu ya wilaya ya Lushoto kuwa awe amekamilisha kazi hiyo baada ya kupewa asilimia 90% ya fedha za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Akizungumza na ITV ofisini kwake kuhusu miradi ya barabara katika wilaya hiyo inavyozorota huku serikali ikiendelea kutoa fedha kwa baadhi ya wakandarasi lakini barabara hizo hazina tija, mkurugenzi wa halmashauriya wilaya ya Lushoto Bwana Jumanne Shauri amesema hadi sasa mkandarasi huyo amekwisha pewa fedha kiasi cha shilingi milioni 240 kati ya shilingi milioni 390 za mradi huo lakini ujenzi huo umechukua zaidi ya mwaka bado kukamilika.
Katika hatua nyingine wilaya ya Lushoto imepata tuzo kwa kushika nafasi ya tatu katika zoezi zima la utunzaji mazingira hatua ambayo imesababisha uoto wa asili katika wilaya hiyo kuanza kurejea baada ya kuanza operesheni ya kupanda miti kuanzia shuleni hadi majumbani kufuatia baadhi ya watu kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara kuharibu vibaya misitu ya asili ya hifadhi katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo waliojikita na mazingira wamesema hivi sasa wanafanya operesheni ya kuwakamata na kuwafikisha katika mabaraza ya kata baadhi ya wakazi ambao hawana vyoo ili kuhakikisha wanaimarisha usafi wa mazingira katika maeneo tofaut wilayani Lushoto.