Wachezaji wa Yanga sasa kuanza mazoezi chini ya Maximo
KOCHA mpya wa Yanga sc, Mbrazil Marcio Maximo ameanza kazi leo kwa kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo .
Mkutano huo umefanyika makao makuu ya klabu ya Yanga, makutano ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es salaam.
Maximo alipata nafasi ya kuwaeleza mipango yake ya kazi na kuwataka wachezaji waelewe umuhimu wao katika kujenga mafanikio ya Yanga.
Kocha huyo aliyewahi kufanya kazi nchini kwa kuifundisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars, baada ya kukutana na wachezaji leo hii, sasa yuko tayari kuanza mazoezi ya kujiwinda na msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza mwezi agosti mwaka huu.
Pia Yanga itashiriki michuano ya kombe la kagame na kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita.
Maximo katika programu yake atakuwa na wachezaji ambao hawako kwenye vikosi vya timu za taifa kujiandaa na michezo ya kuwania nafasi ya kupangwa hatua ya makundi ili kusaka tiketi ya fainali za AFCON mwakani nchini Morocco.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwemo nahodha, Nadir Haroub `Cannavaro`, kipa Deogratius Munish `Dida`, Kelvin Yondani, Oscar Joshua na wengineo wapo na kikosi cha Taifa stars katika kambi ya wiki mbili mjini Gabarone, nchini Botswana.
Wakati Yanga wakifurahia na ujio wa Maximo, kwa upande wa Simba wamekamilisha uchaguzi wao hapo jana.
Evans Elieza Aveva alishinda kwa kishindo dhidi ya Andrew Peter Tupa na kuwa rais wa kwanza wa Simba .
Naye Goefrey Nyange `Kaburu` aliibuka kidedea katika kinyang`anyiro cha umakamu wa rais wa klabu hiyo.
Wajumbe walioshinda na kuingia katika kamati ya utendaji ya Simba sc ni Idd Kajuna, Coliins Friesh, Ally Suru na Saild Tully. Kwa upande wa mwanamke ni Jasmin.