Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwasilisha taarifa ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF Taifa, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akiwasilisha taarifa ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi kadi ya CUF kwa mmoja kati ya vijana wanaomaliza vyuo, katika ukumbi wa Lamada Dar es Salaam.
Na: Hassan Hamad, OMKR.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema mafanikio na changamoto za chama hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita viwe vitendea kazi kwa uongozi mpya wa chama utakaopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho unaoanza rasmi kesho tarehe 25/06/2014.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya kazi za chama kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.Amesema katika kipindi hicho chama kimepata mafanikio makubwa, licha ya kuwepo changamoto nyingi, na kwamba kila mjumbe anapaswa kuzingatia maslahi mapana ya chama na kuweza kutafakari juu ya uwezo wake, uzalendo na uwajibikaji kwa maslahi ya chama hicho.
Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka mitano iliyopita kuwa ni pamoja na kuendelea kumiliki kampuni inayochapisha gazeti la FAHAMU linalochapishwa kila siku ya Jumanne, ambapo kampuni hiyo sasa inakamilisha mchakato wa kukifanya chama hicho kianze kumiliki vituo vya redio kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa chama chake pia kimefanikiwa kushiriki chaguzi mbali mbali zinazofanyika nchini, sambamba na kuendelea kujifunza mabadiliko ya mbinu za uchaguzi kutoka kwa wapinzani wao, na hivyo kujizatiti zaidi katika chaguzi zijazo.Aidha amesema chama hicho kimefanikiwa kufanya ziara kwa asilimia 70 kwa Wilaya za Tanzania Bara na asilimia 100 kwa Wilaya za Zanzibar, zikiwa na lengo la uimarishaji na ujenzi wa chama katika ngazi za chini.
Kuhusu changamoto Maalim Seif amesema ni pamoja na ukosefu wa vyanzo vya mapato ambapo kwa sasa wanategemea vyanzo vichache vya mapato vikiwemo ruzuku kutoka serikalini pamoja na michango ya wabunge na wawakilishi ambavyo havimudu kutekeleza hata nusu ya vipaumbelea vya chama, ukiachilia mbali matumizi ya kawaida ya chama.Hivyo amewataka wajumbe wa mkutano mkuu Taifa kubuni vyanzo vyengine vya mapato ili kuongeza mapato ya chama na kuweza kutekeza majukumu mengi zaidi.
Ametaja changamoto nyengine kuwa ni upungufu wa vitendea kazi vikiwemo vyombo vya usafiri katika ngazi zote za uongozi na hivyo kuzorotesha utendaji wa chama hicho.Aidha amesema baadhi ya viongozi na wanachama wamekuwa wakitishwa, kubambikiziwa kesi na wengine kufungwa, jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo watendaji wa ngazi mbali mbali katika chama.
Mapema wakichangia taarifa hizo za chama, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wamewaomba viongozi wa kitaifa wa chama hicho kufanya juhudi za ziada ili kuhakikisha kuwa wanazitembelea Wilaya zote za Tanzania, bila kujali wingi au uchache wa wanachama katika Wilaya hizo.
Wakati huo huo akizungumza na vijana wa CUF wanaomaliza vyuo vikuu, Maalim Seif ameahidi kuiimarisha Jumuiya ya vijana ya chama hicho (JUVI CUF), ili kuiwezesha kuwa na program endelevu zitakazosaidia kuwajengea uwezo zaidi vijana ili waweze kushika hatamu za uongozi.
Jumla ya vijana 54 wanaomaliza vyuo vikuu walijiunga na CUF kwenye hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Lamada Dar es Salaam, na kuahidi kushirikiana na chama hicho katika kuleta ufanisi zaidi.