Aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Van der Pluijm (wa kwanza kulia) anatarajia kuungana na Mkwasa (wa pili kulia) nchini Saudi Arabia
KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Mtanzania Charles Boniface Mkwasa ametimkia Uarabuni kuungana na aliyekuwa bosi wake msimu uliopita Mholanzi, Hans Van Der Pluijm.
Pluijm baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita Yanga, aliamua kuondoka kwenda Saudi Arabia kuifundisha klabu ya ligi kuu ya Saudi Arabia iitwayo Al Shoalah FC .
Kocha huyo Mholanzi aliondoka kwa makubaliano maalum na Yanga, huku akieleza kuwa wakati anajiunga na Yanga aliwaambia kuna dili anasubiria na kama litakwenda sawa ataondoka.
Baada ya mambo kwenda sawa, aliondoka Yanga na kuagana kwa amani na uongozi wa Yanga pamoja na wanachama.
Pluijm alionekana kumkubali Mkwasa na sasa ameamua kumtafutia kazi nchini Saudi Arabia na kocha huyo Mtanzania anakwea pipa usiku huu.
Kabla ya kukwea pipa, Mkwasa amesema tayari ameshawajulisha viongozi wa Yanga na umetoa Baraka zote na kumpa ushirikiano mzuri.
"Viongozi wamenipa ushirikiano mzuri kwasababu nao wangependa nipate uzoefu hususani kwa klabu za nje. Labda nitakaporudi nitaweza kuisaidia klabu". Alisema Mkwasa.
Hata hivyo, Mkwasa amegoma kutaja timu anayoenda kufanya kazi kwasababu mambo hayajakamilika, lakini mambo yakienda sawa ataanika kila kitu kwa wananchi.
Mkwasa aliongeza kuwa yeye amepata mwaliko baada ya kutuma wasifu wake (CV), ingawa amekiri kuwa hayo yamejiri kutokana na jitihada za aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans Der Pluijm.
Kocha huyo aliyekuwa na Ruvu Shooting mwanzoni mwa msimu uliopita aliongeza kuwa Saudia Arabia ipo juu kisoka ukilinganisha na Tanzania na kizuri zaidi wachezaji wengi wa ulaya wanapochoka huwa wanatafuta nafasi ya kucheza huko, hivyo itampa changamoto mpya.
Mkwasa alifafanua kuwa mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwasababu anaenda kujifunza huko na kuna uwezekano akapangiwa majukumu tofauti na aliyokuwa nayo sasa hivi.
"Naenda kupata uzoefu ambao naamini nitakapoupata, naamini utaisaida Yanga na taifa kwa ujumla". Alihitimisha Mkwasa.
Kila la heri Charles Boniface Mkwasa `Master` katika maisha mapya ya kazi yako huko Uarabuni.