Kampuni ya Statoil na mshirika wake ExxonMobil wamegundua kiasi kingine kikubwa cha gesi katika bahari ya Hindi nchini Tanzania.
Ugunduzi huu unahusisha kisima cha Piri-1 ambapo kiasi kilichopatikana kinakadiriwa kufikia trilioni mbili mpaka tatu za ujazo wa gesi asilia yaani trillion cubic feet (tcf) kwa kiingereza.
Ugunduzi huu unafanya jumla ya ujazo wa gesi iliyogundulika na washirika hawa kufikia takribani tcf 20 kwenye kitalu namba 2 ambapo washirika hawa wanafanya shughuli za utafiti na uchimbaji
''Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukipata mafanikio ya asilimia mia moja nchini Tanzania na eneo hilo limekuwa kitovu cha utafiti ndani ya muda mfupi sana. Ni kwa haraka tulitoka kwenye kuchimba kisima kimoja hadi kuwa na mkakati wa kuchimba visima vingi na Piri -1 ni muendelezo wa mafanikio haya,'' anasema Nick Maden Makamu wa Rais wa shughuli za utafiti za Statoil katika ukanda wa Magharibi.
Ugunduzi huu mpya wa gesi asilia umefanyika katika eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati ilipogunduliwa gesi katika kisima cha Zafarani-1 kilichochimbwa mwaka 2012.
Ugunduzi katika kisima cha Piri-1 unakuwa wa sita katika safari ya ugunduzi katika kitalu namba 2. Piri imetanguliwa na ugunduzi mkubwa kwenye via vya Zafarani-1, Lavani-1, Tangawizi-1, Mronge-1 na Lavani-2.
Uchimbaji wa Piri-1 ulifanywa na meli ya Discoverer Americas. Kisima hiki cha Piri kiko kilometa mbili kusini magharibi mwa kisima cha Lavani-1 kwa usawa wa mita 2,360 za kina cha maji. Meli hii ya Discoverer Americas sasa imehama na inachimba kisima kingine cha Binzari katika kitalu namba 2.
''Eneo lingine la utafiti limeshaandaliwa na litajaribiwa ndani ya mwaka 2014 na 2015. Tunatarajia kuchimba visima zaidi na tunatumaini kuwa matokeo ya visima hivi yataongeza kiasi cha ujazo wa gesi kwa ajili ya miundombinu ya mradi mkubwa wa gesi hapo baade,'' anasema Maden.
Statoil inajihusisha na utafiti wa gesi katika kitalu namba mbili ndani ya bahari ya Hindi kwa niaba ya shirika la maendeleo ya mafuta nchini (TPDC). Statoil ina hisa ya asilimia 65 katika kitalu hicho wakati mshirika wake ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited wanashikilia hisa kwa asilimia 35.
Statoil imekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 2007 ilipopatiwa kibali cha kufanya shughuli za utafiti katika kitalu namba 2.Kwa habari zaidi tembelea; www.statoil.com