Mkuu wa Kitengo cha Risks na Compliance wa Benki ya Exim, David Lusala (wapili kushoto) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa Mweka Hazina wa Tushikamane Pamoja Foundation (TPF), Ana Rupia (wapili kulia), ikiwa ni sehemu ya msaada wa benki hiyo kupiga jeki miradi ya TPF ya kuwasaidia wazee wasiojiweza. Wakishuhudia ni Meneja wa Fedha Mwandamizi wa Benki ya Exim, Issa Hamisi (katikati) na Meneja Masoko Msaidizi wa Benki hiyo Anita Goshashy
Mkuu wa Kitengo cha Risks na Compliance wa Benki ya Exim, David Lusala (wapili kushoto) akionyesha hundi ya shilingi milioni 10 baada ya kukabidhi hundi hiyo kwa Mweka Hazina wa Tushikamane Pamoja Foundation (TPF), Ana Rupia (wapili kulia), ikiwa ni sehemu ya msaada wa benki hiyo kupiga jeki miradi ya TPF ya kuwasaidia wazee wasiojiweza. Wakishuhudia ni Meneja wa Fedha Mwandamizi wa Benki ya Exim, Issa Hamisi (kulia) na Meneja Masoko Msaidizi wa Benki hiyo Anita Goshashy (kushoto).
BENKI ya Exim Tanzania imekabidhi hundi ya shilingi milioni kumi kwa taasisi ya Tushikamane Pamoja Foundation (TPF) ikiwa na lengo la kusaidia wazee wasiojiweza wanaoishi katika kaya zaidi ya 40 jijini Dar es Salaam.
Taasisi hiyo ambayo kwa sasa inasambaza chakula na vitu binafsi kwa kaya 40 jijini Dar es Salaam kila mwezi pia utekeleza miradi mbali mbali ambayo ni pamoja na matibabu kwa kundi hilo maalum.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Risks na Compliance wa Benki ya Exim, David Lusala alisema kuwa benki inajua umuhimu wa kuchangia sehemu ya pato lake kwa jamii, kwa njia ya miradi ambayo inabadilisha au kuboresha viwango vya kijamii na kiuchumi kwa jamii.
"Benki ya Exim imekuwa makini sana katika kusaidia jamii ianyoizunguka. Kama sehemu ya shughuli zetu za kijamii, leo tunakabidhi shilingi milioni 10 kwa taasisi ya TPF ili kupiga jeki miradi yao iliyoanzishwa ili kusaidia wazee wasiojiweza na jamii kwa ujumla.
"Nauasa uongozi wa TPF kuhakikisha kuwa fedha hizi tulizochangia zinaelekezwa kwenye matumizi yaliyokusudiwa ili kuwawezesha watu wasiojiweza kufaidika na shughuli zenu zenye malengo mazuri ya kuboresha maisha yao," alisema Bw Lusala.
Alibainisha kuwa benki ya Exim itaendelea kuelekeza fedha zake katika kusaidia miradi ambayo ni chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini ili kusaidia kuboresha hali ya maisha ya jamii.
Kwa upande wake, Mweka Hazina wa Tushikamane Pamoja Foundation, Bi. Ana Rupia ameipongeza Benki ya Exim kwa msaada wake na kusema kuwa fedha hizo zilizopokelewa na TPF zitaelekezwa katika miradi ambayo tayari iliyoundwa kwa lengo la kuwasaidia wazee wasiojiweza.
"Tuna mpango wa kujenga nyumba kwa ajili ya wazee katika kata ya Kwembe, Wilayani Kinondoni ambayo itakuwa kama makazi ya wazee wasiojiweza. Nyumba hiyo itatoa urahisi wa wazee hao kupata huduma za matibabu, usimamizi wa karibu na huduma nyingine za kiubinadamu kwa walengwa.
"Sasa tunasubiri kibali cha ujenzi kabla ya kuanza kazi ya ujenzi rasmi. Tunaishukuru Benki ya Exim kwa msaada wao na nazisihi taasisi nyingine kuiga mfano huu mzuri wa kuigwa," Bi Rupia alisema.