UMOJA wa Katiba ya Wananchi ( UKAWA ) umepokelwa kwa mabango yanayowapinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa yaliyokuwa yamebebwa na vijana.... Mabango hayo yalikuwa yanasomeka kuwa, "Tuna mashaka na ndoa ya UKAWA watauza nchi", huku yakisisitiza umuhimu wa vijana wa Wilaya ya Mufindi kutaka Serikali mbili.....
Pia mabango hayo yalikuwa yanawataka wajumbe wa UKAWA warudishe posho kwanza bungeni mjini Dodoma....
Katika mkutano wao uliofanyika juzi mjini Mafinga Viwanja vya mashujaa, mkutano huo uliendeshwa na mwenyekiti wa chama cha Wananchi ( CUF ) ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa UKAWA.....
Wengine waliohutubia ni pamoja na mwakilishi wa chama cha NNCR-Mageuzi,Danda Juju na kiongozi wa taasisi ya kiislam ya Shura ya Imamu,Rajabu Katimba.
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na vijana hao wilayani Mufindi yalikuwa na ujumbe uliosomeka: "Vijana Mafinga tuna mashaka na ndoa ya UKAWA,watauza nchi" na bango la waendesha bodaboda lilisomeka: "Rudisheni posho kwanza mjengoni Dodoma"
Mengine na ujumbe wake kwenye mabano ni lililowatambulisha wafanyabiashara wa sokoni lililosomeka, "Mafinga Sokoni,Serikali tatu siyo suluhisho la matatizo ya wananchi", na la wapiga debe mafinga stendi lilisomeka, "Karume Oyee, Nyerere Oyee, Muungano Saafi!".
Bango la waliojitambulisha kuwa ni machinga lilisomeka,"Tunataka Serikali inayojali wajasiriamali, siyo kujali matumbo yao"...Na lile la wakulima lilisomeka, "Kilimo Kwanza, Utaifa kwanza".
Wakati mabango hayo yakizungushwa katika mkutano huo muda ambao Profesa Lipumba alikuwa akihutubia, usikivu ulipotea kwa takribani dakika 15 hadi 20 baada ya sehemu ya kundi la vijana lililokuwa likimsikiliza kuelekea upande walikokuwa vijana wenye mabango hayo....
Polisi waliokuwepo walilazimika kuingilia kati kadhia hiyo na mzozo huo baina yao na vijana waliokuwa na mabango ulisikika....
Mmoja wa polisi aliyekuwa akiwatuliza vjana hao alisema,"Jamani huu ni mkutano halali wa kisiasa, acheni wenzenu wafanye mkutano wao, yatoeni mabango yenu"
Mmoja wa vijana aliyekuwa amebeba bango mojawapo jina halikupatikana mara moja alisikika akisema, "UKAWA siyo chama cha siasa, wao wanamtazamo wao na sisi tuna mtazamo wetu, kwa hiyo siyo jambo la ajabu wakajua kwamba Mafinga wengi hatuwaungi mkono na siyo dhambi kuonyesha hisia zetu katika mkutano wao"
Akielezea vurugu hizo, profesa Lipumba alisema zinafanywa na vijana waliotumwa na CCM kwa sababu ya msimamo wao wa kutaka serikali mbili, tuhuma zilizokanushwa na katibu wa CCM wilaya ya Mufindi,Miraji Mtaturu aliyehojiwa baada ya mkutano huo...
"Siamini kama mkutano huu ungekuwa unahutubiwa na mwenyekiti wa CCM wa taifa Jakaya Kikwete wangekuja na mabango yao na kufanya vurugu hizi," alisema Lipumba na sauti toka kwa baadhi ya vijana hao zikasikika zikisema, "Kama angekuja na msimamo wa serikali tatu ni lazima angekutana na mabango haya, sisi tunataka serikali mbili"
Hata baada ya vurugu hizo kutulia na Profesa Lipumba kuruhusu maswali baada ya kufafanua sababu mbalimbali zilizowafanya wasusie bunge la katiba na kuanzisha UKAWA, mkutano huo ulitaka kuvurugika tena....
Swali liliotaka kuuvuruga mkutano huo lilitoka kwa kijana aliyejitambulisha kwa jina la Rahid Rashid ambaye alitaka kujua kwa nini CCM hawapo katika umoja huo.
Pamoja na vijana wengine kupiga kelele wakiashiria kuwa hilo siyo swali,Profesa Lipumba alijibu na kusema hilo ni swali zuri.
Alisema milango ya UKAWA ipo wazi kwa mtu yeyote ndani na nje ya bunge la katiba wakiwemo wabunge na viongozi wa CCM
"Tutafurahi kuwapata wana CCM,tunawakaribisha UKAWA ili kwa pamoja tushirikiane kupata katiba inayotokana na wananchi,"alisema
Mwingine aliyeuliza swali alikuwa Winfrida Ngoti aliyesema harakati za kudai serikali tatu hazitakuwa na maana yoyote kama matatizo ya wananchi hayatashughulikiwa.
"Watanzania wana matatizo lukuki,vituo vya huduma za afya havina wataalamu,dada,wakulima hawapati pembejeo kwa wakati na bei zake ni kubwa, wafanyabiashara wadogo wanabanwa na kukamuliwa kodi, walimu haapati mishahara kwa wakati, askari wana mishahara midogo ," alifafanua
Katika majibu yake, profesa Lipumba alisema hayo yote yatafanyiwa kazi kukiwa na katiba bora itakayosisitiza uwajibikaji na uadilifu.