Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu sita wanaodaiwa ni viongozi wa kundi la 'Mbwa Mwitu' linalojihusisha na vitendo vya uvamizi na uporaji wa mali za watu kwenye nyumba na maduka jijini humo.
Kamanda wa olisi kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema kutokana na kukamatwa kwa viongozi hao na kupatikana kwa taarifa za makundi hayo jeshi lake litafanya msako wa nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa hadi wahusika wote wakamatwe.
Hawa viongozi tunao, tumeshawahoji na wamekiri ni kweli wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kwa kutumia makundi yao," alisema Kova na kuongeza: "Sisi tunaanza kuwasaka hao vijana kwa sababu tumeshapata taarifa za kutosha kutoka kwa wenzao…tunafahamu wapi pa kuwapata."
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Athuman Said (20), Joseph Ponela na Clement Peter (25) wakazi wa Kigogo, Roma Vitus (37), Mwanshishe Adam(37) na Daniel Peter (25)wakazi wa Temeke.
Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya kusambaa kwa taarifa za kundi hilo la vijana zaidi ya 300 kuvamia mitaa mbalimbali ya jiji hilo, kupora mali na kujeruhi watu.
Kamishna Kova alisema kuwa jeshi lake lilifanikiwa kuwakamata viongozi hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema akisisitiza kwamba hatua inayofuata ni kuwasaka vijana wanaowatuma kufanya uhalifu huo.
"Hii itakuwa operesheni endelevu tunayoianza mwezi huu hadi mwezi Julai mpaka tuhakikishe tumewakamata wahalifu hawa na tatizo hili limetokomea,"alisema Kova kwa msisitizo.
Alisema jeshi lake limejipanga kukabiliana na wahalifu hao na kuwa wananchi waache kuwa na hofu kutokana na taarifa za uvumi zinazosambazwa kwenye mitandao kuhusu uhalifu unaofanywa na vijama hao.
"Ningependa kuwatoa hofu wananchi kuhusiana na uvumi unaoendelea kwenye mitandao…tunaomba wananchi wawe watulivu waendelee na shughuli zao kama kawaida. Jeshi langu limejipanga vizuri kuwadhibiti hao vijana. Hao vijana hawana uwezo wa kutushinda sisi" alisema Kova
Kamanda huyo aliweka wazi kuwa askari wa kutosha wa doria wameshapangwa maeneo ambayo yametajwa kuwa na mlipuko wa makundi hayo.Maeneo hayo ni pamoja na Kigogo, Manzese, Magomeni na Mbagala.
Mwananchi