MWILI wa mwimbaji nyota wa kike wa muziki wa dansi, Amina Ngaluma aliyefariki Alhamisi iliyopita, utawasili nchini Ijumaa usiku.
Mume wa marehemu, Rashid Sumuni ameiambia Saluti5 kuwa mwili wa mkewe aliyefia nchini Thailand, utasafirishwa kwa ndege ya KLM na kutua jijini Dar es Salaam uwanja wa ndege wa kiamataifa wa Mwalimu JK Nyerere Ijumaa usiku.
Sumuni amesema kama taratibu zote zitakwenda kama zilivyopangwa, basi Amina Ngaluma atazikwa Dar es Salaam Jumamosi.
Kwasasa msiba wa Amina Ngaluma unaendelea nyumbani kwa baba yake Kitunda jijini Dar es Salaam.
Mwanzoni ilielezwa kuwa mwili wa Amina Ngaluma utaondoka Thailand Jumatatu na kupokelewa Dar es Salaam Jumanne.
Wakati Sumuni akiyasema hayo, msanii mwingine wa kike aliyekuwa akifanya kazi pamoja na Amina Ngaluma huko Thailand, Easter Lazaro, hadi Juzi Jumapili alikuwa hajui kinachoendelea.
Easter aliyekuwa wa kwanza kutoa taarifa za kuugua kwa Amina Ngaluma kupitia Facebook, amekuwa na majibu mafupi kupitiliza kila anapoulizwa kinachoendelea huko Thailand. Tarehe 15 alisema "Tutatawajulisha kesho". Alipoulizwa na Saluti5 Jumapili kuna jipya gani huko akajibu "Hakuna". Lakini hata pale alipoambiwa kuwa huku Dar es Salaam tunatangaziwa kuwa mwili utaingia Jumanne na kutakiwa afafanue kama hilo lina ukweli akasema "Sijui".
Kwa majibu hayo ya Easter ambaye ni mmoja wa Watanzania wanaoshughulikia taratibu za kuuleta mwili wa Amina Ngaluma, haitakuwa ajabu kama yatatokea mabadiliko mengine.