Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ameitaka Bodi ya Usajili ya Makandarasi Tanzania (CRB), kuwabana na kuwafutia usajili makandarasi ambao hawafuati na kuzingatia sheria za ujenzi.
Pia, Ndikilo ametaka makandarasi wenye tabia za kutumia majina ya kampuni kubwa za ujenzi kwa lengo la kupata zabuni za miradi, waache tabia hiyo kwani wakibainika wachukuliwe hatua kali za kisheria kiwamo kufutiwa usajili.
Akifungua mkutano wa bodi ya CRB jana, Ndikilo alisema majengo mengi yamekuwa yakiporomoka kwa sababu ya makandarasi kutozingatia sheria za ujenzi, jambo ambalo ni vyema bodi ikaliangalia kwa kina.
"Bodi ina kazi kubwa ya kuhakikisha makandarasi ambao hawana vigezo vya kupewa zabuni kubwa hawapewi na kwamba, sheria za ujenzi lazima zisimamiwe ipasavyo ili kupunguza maafa yanayotokana na kuporomoka kwa majengo," alisema Ndikilo na kuongeza:
"Kuna baadhi ya makandarasi ambao hawana sifa wamekuwa wakitutumia majina ya kampuni kubwa kupata zabuni, naomba watu hawa wakibainika wafutiwe vibali vyao mara moja ili tuongeze ufanisi katika sekta ya ujenzi nchini."
Ndikilo alisema ni vyema makandarasi wakaacha tabia ya kukimbilia kazi kwa sababu ya uchu wa kupata fedha, bali wafanye kazi kulingana na uwezo wao.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Boniface Muhegi alisema mwaka jana makandarasi 752 walifutiwa usajili kutokana na kukwepa kulipa ada na kodi mbalimbali za Serikali.
Mhegi alisema makandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ili kuaminika na kwamba kufanya hivyo watakabiliana na vitendo viovu sekta ya ujenzi.
"Kutokana na tabia ya makandarasi kukwepa kulipa kodi na ada za usajili, tumewafutia usajili 752 na wanane walifutwa kutokana na kutokumaliza kazi," alisema Muhegi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi