Baba mzazi Kolinel Mushin kushoto akimsikiliza mkewe kwa makini baada ya mama huyo kufika kijijini kwao
Mtoto Selemani Kolineli Mushin(Miezi kumi)kutoka Kijiji cha Igundu Kata ya Sangambi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya amerejea salama Kijijini baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na kuzaliwa na matatizo ya mdomo sungura.
Mtoto huyo alifichwa ndani baada ya kuzaliwa na kutakiwa kurudi Hospitali ya Wilaya ya Chunya miezi sita baadaye lakini Baba Mzazi wa mtoto huyo aitwae Kolineli Mushin akikataa kumpeleka Hospitali akidai huo ni mpango wa Mungu.
Mwanzoni mwa mwezi Mei baada ya mtoto huyo kukutwa na mwandishi wa Mbeya yetu na kuwashauri wazazi wa mtoto ndipo walipokubali kumpeleka Hospitali ambapo dhamana hiyo ilichukuliwa na Afisa Ustawi wa jamii Anna Geleta la kusafirishwa hadi Hospitali ya CCBRT.
Selemani baada ya kupokelewa katika Hospitali ya CCBRT alifanyiwa upasuaji na kurekebishwa mdomo ambao ulikuwa ukimpa shida wakati wa kula na kupumua kwa shida na aliruhusiwa kutoka Hospitali Mei 15 Mwaka huu na kurejea Mbeya Mei 17 ambapo gharama za safari ya kwenda na kurudi na matibabu kugharamiwa na CCBRT.
Kwa upande wake Baba mzazi Kolinel Mushin na Mkewe Yohana Kolineli wameishukuru Mbeya yetu blog, Serikali na Asasi ya CCBRT kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wao ambapo wao walidhani kuwa ugonjwa huo usingetibika.
Aidha walimshukuru msamaria mwema Osward Mwailomo aliyetoa taarifa kwa mwanahabari na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu kwa ushirikiano wake hata kufanikisha upasuaji wa mtoto na hali yake inaendelea vema.
Selemani atafanyiwa upasuaji wa pili mwezi Mei mwakani katika Hospitali hiyo ya CCBRT ambapo gharama zote hutolewa na Hospitali hiyo.
Na Mbeya yetu |