Thursday, November 01, 2012

Yanga yaikamata Simba kileleni.



DHAMIRA ya Yanga kuwatibulia Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, ilishika kasi zaidi jana kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Mgambo, huku Simba waking'ang'aniwa na sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Moro.Ushindi wa Yanga umewafikisha pointi 23, sawa na mahasimu wao Simba wanaoendelea kuongoza msimamo kwa faida ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Sare hiyo ya tano kwa Simba tangu kuanza kwa msimu, ilimkasirisha Kocha Milovan Cirkovic, huku pia akimtupia lawama mwamuzi Jacob Odongo.Kocha Cirkovic hajawahi kukosa kuwalalamika waamuzi kwenye mechi zote ambazo timu yake ilishindwa kupata ushindi.

Katika mechi 11 walizocheza Simba, hawajawahi kupata ushindi nje Dar es Salaam zaidi ya sare mbili Mkwakwani, Tanga na jana Jamhuri, Morogoro.

Kiungo Amri Kiemba aliokoa Simba na kipigo kwa kufunga bao la kusawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Kiemba alifunga bao hilo likiwa la tano kwake msimu huu, akiunganisha wavuni mpira wa kona uliopigwa na Emmanuel Okwi.
Simba walikosa mabao dakika ya 37, 62 na 75 kupitia Okwi na Kiemba, huku Polisi wakishindwa kutungua nyavu za Kaseja dakika ya 28, 60 kupitia Mokili na Malimi Busungu.
Polisi waliwaduwaza Simba kwa bao la kwanza dakika ya 33 likifungwa na Mokili Lambo, aliyetumia dakika tano tu uwanjani alipoingia kuchukua nafasi ya John Bosco dakika ya 28.
Simba walimpumzisha Mrisho Ngassa na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Okufo (57), Komabil Keita badala ya Said Nassor.
Kipa Kaseja alionywa kwa kadi ya njano na mwamuzi, Jacob Odongo kutoka Mara kufuatia kuchelewesha muda katika dakika ya 74.
Kocha Msaidizi wa Polisi, Ally Jangalu aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango kizuri na kuwabana Simba.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Nadir Horoub aliifungia Yanga bao la mapema dakika ya pili akimalizia wavuni mpira wa adhabu uliopigwa na Athuman Idd 'Chuji'.
Kabla ya bao hilo, Hamis Kiiza angeweza kuifungia Yanga bao la utangulizi dakika ya kwanza kama siyo kumalizia vibaya pasi ya Saimon Msuvu.
Mashambulizi ya Yanga pia yalishindwa kuzaa mabao katika dakika ya 11 na 15 kupitia kwa mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Shambulizi pekee la nguvu lililofanywa na JKT Mgambo lilikuwa katika dakika ya 27 kupitia Yasin Awadh aliyeshindwa kuunganisha wavuni mpira wa kona uliochingwa na Bakar Mtama.
Kavumbagu alifunga bao la pili dakika ya 39 baada ya kazi nzuri ya Kiiza aliyewapangua mabeki wa Mgambo, na Jerry Tegete akamaliza kazi kwakupachika bao la tatu kwa shuti la karibu na lango dakika ya 79.
Haruna Niyonzima na Kiiza wangeweza kufunga mabao zaidi kama wangetumia vizuri nafasi walizopata dakika ya 46 na 56.
Kocha wa Yanga Ernest Brandts ameendelea kusifu kiwango cha wachezaji wake, huku kocha wa Mgambo Mohamed Kampira akiwalaumu mabeki wake kufanya makosa yaliyowapa wapinzani wao fursa ya kufunga.
Katika mchezo mwingine kwenye Uwanja wa Chamazi, African Lyon iliendelea kugawa pointi baada ya kunyukwa mabao 4-2 na JKT Ruvu, huku mshambuliaji Mussa Mgosi akifunga bao la nne likiwa la kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo.
Mabao ya washindi yalifungwa na Hussein Bunu (9,45) na Sosthenes Manyasi, huku mabao ya Jacob Masawe (24) na Willian Silvester (68).
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Jesca Nangawe na Lilia Lucas (Morogoro).