Thursday, November 08, 2012

TAMKO LA MKUU WA MKOA WA DODOMA KWA WATOA HUDUMA ZA USAFIRI




Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehama Nchimbi (pichani) amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Makampuni ya usafirishaji abiria (mabasi) yanayoendelea kufanya shughuli ya kupakia na kushusha abiria kwenye maeneo ya katikati ya mji wa Dodoma yasiyoruhusiwa na Mamlaka zinazohusika na badala yake kuagiza shughuli hizo zifanyike katika stendi ya muda iliyopo uwanja wa Maonesho ya Nane Nane Nzuguni.
Dr. Nchimbi amesema kuwa agizo hili linayahusu makampuni yale ambayo hayana vituo rasmi vinavyotambuliwa na kuruhusiwa kisheria na Mamlaka husika (H/M Dodoma) kuendesha shughuli hizo na badala yake shughuli hizo zinatakiwa kufanyika katika Stendi ya Muda iliyopo viwanja vya Nzuguni.
Katika hatua nyingine Dr. Nchimbi amepiga marufuku tabia ya Magari Makubwa ya mizigo kuweka vituo na kuegesha katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma yasiyo rasmi kufanya shughuli hiyo na yasiyoruhusiwa kisheria na Mamlaka husika na badala yake amewataka madereva wa magari hayo kuegesha katika eneo maalumu lililopo kizota lililoandaliwa na Manispaa ya Dodoma na CDA kwa ajili ya shughuli hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo leo ofisini kwake alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari ambapo alisema amewaagiza Manispaa ya Dodoma, Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu (CDA), Polisi – usalama barabarani, wenye makampuni ya usafirishaji na wadau wengine wote wanaohusika kusimamia na kutekeleza agizo hili.
Dr. Nchimbi alibainisha kuwa kwa sasa Mkoa wetu wa Dodoma kupitia Halmashauri ya Manispaa Dodoma na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu – CDA umebahatika kuingia klwenye mpango wa uboreshaji Majiji ambapo Mkoa wa Dodoma umepatiwa zaidi ya shilingi bilioni 30 ili kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara na vituo vya mabasi ya Mikoa na daladala.
Hivi sasa mradi wa uboreshaji kituo cha mabasi ya mikoani unaendelea na Mkataba unamtaka mkandarasi kumaliza kazi hiyo ifikapo mwezi Mei, 2013 lakini kwa kutambua umuhimu wa kituo hiko mkandarasi ameahidi kumaliza kazi hiyo ifikapo Aprili, 2013. Kutokana na ukarabati huo Mamlaka husika (Manispaa Dodoma) imehamishia shughuli zote zilizokuwa zikifanyika kituoni hapo kituo cha Muda Nzuguni na kupiga marufuku shughuli hizo kufanyika katikati ya mji agizo ambalo baadhi ya makampuni yanakiuka.
Kwa upande mwingine Dr. Nchimbi ameeleza kuwa madereva wa magari makubwa ya mizigo wanakiuka kuegesha magari yao eneo la kizota lililotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo badala yake wanaegesha kandokando ya baadhi ya barabara, kwenye mitaa mbalimbali, kwenye vituo vya kuuzia mafuta na kwenye maeneo yakuoshea magari ambapo baadhi yake siyo vituo rasmi.
Dr. Nchimbi amesema tabia hiyo inachangia uharibifu wa miundombinu, uchafuzi wa mazingira, haizingatii taratibu nzuri za mipangomiji na inapoteza mapato kwa mamlaka husika na hivyo inarudisha nyuma juhudi za wadau wengine wa maendeleo na hasa uongozi wa Mkoa wa Dodoma wa kuufanya Mji wa Dodoma kupata hadhi ya kuwa Jiji.
Imetolewa na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
DODOMA