Tuesday, October 16, 2012

ZAMBI AWA MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MBEYA



·     * Wabunge wenzake washangilia
·       * Ngumi zapigwa wajumbe mamluki

Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki Godfrey Zambi ameshinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya.
Zambi kapata kura 888  na kufuatiwa na Allan Mwaigaga ambaye amepata kura 318 na kufuatiwa na Reginald Msomba aliyepata kura 237


Adam Malima ndiye alikuwa msimazi wa uchaguzi huu akitangaza matokeo


Mwenyekiti  mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mbeya, Nawab Mullah, akimkaribisha mwenyekiti mpya

Allan Mwaigaga ambaye amepata kura 318 na kuwa mshidi wa pili akiwashukuru wanachama wa ccm katika uchaguzi huo na kusema sasa makudi yavunjwe maadam mshindi kapatikana 


Reginald Msomba aliyepata kura 237. mshindi wa tatu nae pia akiwashukuru wanachama wa ccm katika uwanja wa sokoine jijini mbeya

Mkuu wa mkoa Mbeya Abasi Kandoro kulia katikati  chales Mwakipesile kushoto kabisa mwenyekiti mstaafu mulla wakiwa makini kufuatilia matokeo uwanjani hapo  mida ya saa sita kamili usiku


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima akimsisitizia jambo fulani mwenyekiti mpya wa ccm mkoa wa mbeya G. Zambi


Na, Gordon Kalulunga

MBUNGE wa Jimbo la Mbozi Mashariki Godfrey Zambi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupata kura 888.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya na kuwahusisha wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Mbeya kutoka kila kona ya mkoa huo, kulijitokeza vituko kadhaa ukiwemo ugomvi kati ya wajumbe halali na Mamluki.

Ugomvi huo ulizuka katika jukwaa la wajumbe wa wilaya ya Mbozi ambako wajumbe 15 walibainika kuwa hawakuwa wajumbe halali hali ambayo ilisababisha mkutano kusimama kwa muda kabla jambo hilo halijasuluhishwa.

Akitatua tatizo hilo, Msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Adam Malima alilazimika kumwita Katibu wa CCM wilaya ya Mbozi ambaye alilazimika kumpatia majina ya wajumbe ambao walikuwa wakilalamikiwa ndipo akatangaza kuwa wajumbe hao walitakiwa kutoka nje ya uwanja na wakatii amri hiyo kabla majina yao hayajasomwa hadharani.

Malima aliwaambia wajumbe hao kuwa kinachoitafuna CCM ni makundi ya wao kwa wao hivyo aliwataka kuungana na kuwachagua viongozi ambao wataweza kumaliza makundi yao ndani ya chama hicho.

Uchaguzi uliopoanza na wajumbe wakiwa wanapiga kura, alijitokeza Waziri wan chi ofisi ya Rais Stephen Wasira ambaye baada ya kupokewa alipewa nafasi ya kusalimia na kueleza machache.

Waziri Wasira alisema kuwa wanachama na viongozi wa CCM wanatakiwa kujibu mapigo ya vyama vya upinzani kwa hoja kila inapobidi badala ya kulalamika kuwa wanasingiziwa.

‘’Vyama hivi vingine ni vya msimu na wanasubiri mpaka jambo litokee ikiwemo misiba ndipo wajitokeze kusema uwongo, lakini wanaCCM tunatakiwa kuwajibu kwa kusema ukweli’’ alisema Wasira huku akishangiliwa.

Baada ya kura kuhesabiwa, Msimamizi wa uchaguzi huo Adam Malima alimtangaza Godfrey Zambi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya ambaye alipata kura 888, akifuatiwa na Allan Mwaigaga ambaye alipata kura 318 na kufuatiwa na Reginald Msomba aliyepata kura 237

Katika uchaguzi huo, Wabunge wa CCM kutoka katika baadhi ya majimbo ya mkoa wa Mbeya walijitokeza huku wakionekana kuwa na furaha tangu walipofika uwanjani na hata kabla matokeo hayajatangazwa ambapo ilielezwa kuwa walijua matokeo yatakayotangazwa kutokana na wao kumuunga mkono Mbunge mwenzao.

Wabunge ambao walikuwepo ni Mbunge wa Jimbo la Songwe Philip Mullugo, Jimbo la Kyela Dr. Harrison Mwakyembe, Mbarali Dickson Kilufi na Jimbo la Mbeya Vijijini Mch. Luckson Mwanjale.