Friday, October 05, 2012

Wizara ya Nishati na Madini yawanoa waandishi wa habari



Wizara ya Nishati na Madini imeandaa ziara ya mafunzo kwa waandishi wa habari katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuwapa fursa ya kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara hiyo.
Msemaji wa Wizara, Bw Fadhil Kilewo amesema waandishi wanaoshiriki katika ziara hiyo watasaidia kufikisha taarifa kwa watanzania kuhusu shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara yake katika Kanda ya Kusini.
Aidha, Bw Kilewo ameongeza kuwa waandishi hao pia watapata fursa ya kuzungumza na wananchi katika maeneo husika kusikia maoni yao juu ya huduma zitolewazo na wizara hali itakayowawezesha kutoa taarifa sahihi kwa pande zote mbili yaani serikali na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Ziara hiyo ya siku kumi ilianza tarehe moja mwezi huu wa Oktoba, ikiwa ni mwendelezo wa mikakati mahsusi na endelevu ya wizara kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu kazi inazofanya na pia kusikia maoni kutoka kwa wananchi ili kuboresha utendaji wake.
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Kaimu Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Mtwara, Bw Daniel Kiando kuhusiana na mradi wa umeme wa uhakika vijijini unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia. Hapa ni Kijiji cha Mbambakofi, Mtwara Vijijini.

Mkazi wa Kijiji cha Mbambakofi, Mtwara Vijijini, Aisha Laisi (Mwenye ushungi) akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari. Bibi Aisha amesema amefarijika sana na punguzo la kuunganishiwa umeme lililotolewa na Serikali kwa Vijiji vya Lindi na Mtwara.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mtwara, Bw Daniel Kiando akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mbambakofi na kuwasisitiza watumie fursa ya punguzo la umeme iliyotolewa na Serikali kuunganisha umeme katika makazi yao kabla ya muda uliotolewa kuisha.
Transfoma yenye uwezo wa kubeba umeme wa Kilovolti 25 katika Kijiji cha Mbambakofi. Kwa mujibu wa Meneja Kiando, kiasi hicho cha umeme ndicho kinachohitajika kwa matumizi ya kijiji hiki.
Mkazi wa Kijiji cha Mbambakofi, Hamidu Selemani akiwa nje ya nyumba yake. Bw Selemani amekamilisha taratibu zote za kufungiwa umeme na ni miongoni mwa wakazi watakaonufaika na punguzo la gharama za kuunganishiwa umeme.
Nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Nanyamba Wilaya ya Tandahimba iliyonufaika na Mradi wa Umeme Vijijini. Nyumba hii inatumia mita ya Luku.
Kazi ya kusimika nguzo ikiendelea katika moja ya vijiji vitakavyonufaika na Mradi wa Umeme Vijijini.
Msemaji wa Wizara, Bw Fadhil Kilewo akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa waandishi wa habari katika ziara hiyo.