Wednesday, October 17, 2012

DIALLO MWENYEKITI MPYA CCM MWANZA, MABINA KUKATA RUFAA KUPINGA MATOKEO .....!!!



Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, na mbunge wa zamani wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza, Anthony Mwandu Diallo, ameibuka mshindi kwa kura 611 katika wa nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, kisha kumgalagaza aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Clement Gregory Mabina aliyepata kura 328.

Pichani Wadau wa uchaguzi wa mkutano mkuu wa mkoa wa mwanza wakijipanga kabla ya uchaguzi huo uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

 Wajumbe kupitia utaratibu uliowekwa walijipanga kwenye mistari kwenda kupiga kura kuchagua viongozi nafasi mbalimbali.

 Huu ndio utaratibu wa zoezi la kupiga kura katika Mkutano mkuu wa mkoa wa Mwanza.

 Kisha unatumbukiza hapa kwenye vyombo hivi vya wazi...

 Zoezi gumu la uhesabu kura ukafuata....

 Wajumbe wakaserebuka kusubiri matokeo ingawa simu zilizuiwa kuingia kwenye chumba cha kuhesabu kura.. lakini wapi...!!  Habari zilipenya, mara tetesi kwa upande wa magharibi wakiwa wamenuna kumaanisha kuwa imekula kwao, nao mashariki wakifunguka kwa matabasamu kumaanisha yaliyomo yamo, ukiuliza aku tunafurahia muziki...tehe-te...

 Dj Chris kutoka Semira mobile Sound ndiye aliyekuwa akimwaga burudani kwa wajumbe kuvuta subira kungoja matokeo rasmi kutangazwa....kulikuwa hakuna pombe lakini watu walilewa.

 Wakati huo wajumbe wakifuatilia matukio mbalimbali ya mkutano huona habari nyinginezo duniani kupitia www.gsengo.blogspot.com

Mbali na Diallo, wagombea wengine wa nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, waliotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na Bunge, William Lukuvi ni pamoja na Zebedayo Athumani (kura 4), Hussein Mashimba (kura15), Joseph Langula Yared (kura 30), na Mabina ambaye alipata (kura 328) wote kati ya kura zote 988 halali zilizopigwa.


Wakati wa kutoa shukurani mwenyekiti aliyekuwa akitetea kiti hicho na kuangushwa Mh. Clement Mabina mbali na kupinga matokeo hayo waziwazi akidai kuwa atakwenda kukata rufaa,  ilidaiwa kuwepo kwa mchezo mchafu ambapo mmoja wa wagombea alidaiwa kutoa rushwa ya sh. 50,000 kwa kila mjumbe, kati ya wajumbe wanaokadiriwa kufikia 988, na kwamba inadaiwa kigogo huyo alitumia zaidi ya sh. Milioni 56 kwa lengo la kutafuta ushindi wa nafasi uenyekiti.


Maneno hayo yaliifanya meza kuu kuwa na tafakuri za kina huku minong'ono ya hapa na pale ikitawala... sssssSSSSSsssss!!!... sikiliza kesho Amlifaya na Millard Ayo.

Diallo akitoa neno la shukurani...

Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama na kusema kuwa mkutano huo ni halali na umefuata taratibu zote hivyo kama Mabina anadai kuwa si halali kwa vigezo alivyotaja basi akate rufaa na tume ya uchunguzi haito bagua kukagua mgombea anayelalamikiwa tu! bali itakaguwa wagombea wote wa nafasi ya U-enyekiti mkoa.

Viongozi ambao pia ni wajumbe wa mkutano huo toka kada mbalimbali wakifuatilia hitimisho la mkutano huo ndani ya dimba la CCM Kirumba MZ.

Mwenyekiti mpya Dr. Anthony Diallo akizungumza na waandishi wa habari.

Uchaguzi huo ulifanikiwa pia kuwachagua wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza, ambapo waliochaguliwa na wilaya wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Mwamba Makune na Christine Mwalu Jilala (Misungwi), Joseph Langula Yared na Marco Mabihya (Sengerema), Stella Aya, Raban Mageje (Magu).


Wengine ni Angelina Mabula, Dede Swila (Ilemela), Sikitu Sanziyote na Charles Marwa Nyamasiriri (Nyamagana), George Nyamaha na Benadethar (Ukerewe), huku wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza wilaya Kwimba waliochaguliwa ni Bujiku Philip Sakila na Dominic Kadaraja.